Haya yamezungumzwa na Mgeni rasmi wa hafla ya maadhimisho ya siku ya wazee Duniani, Mhe. Katule G. Kingamkono ambae ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kyela, tarehe 01/10/2023.
Akitoa Hotuba yake katika viwanja vya KYECU vilivyopo kata ya Ipinda wilayani Kyela ,Mhe. Katule amesema, Ni muhimu wazee wakafanya mazoezi ili kulinda afya zao, kwa sababu mazoezi ni tiba tosha ya kuzuia magonjwa.
Amewataka wazee kufanya mazoezi ya kutembea kwa kuzunguka maeneo ya nyumba zao au kufanya matembezi mafupi ili kuulinda mwili na kuepukana na magonjwa ya uzeeni.
Pia amewakumbusha wazee kula vyakula vya asili zikiwemo mbogamboga na matunda ya asili kwani vyakula hivyo vina virutubisho vya kutosha.
Wazee wakiwa wamejipanga tayari kwa mashindano ya kufukuza kuku
Mheshimiwa Katule ametoa shukrani kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwakumbuka wazee na kuwapa huduma za afya Bure kwa kupitia dirisha maalumu la wazee katika vituo vya kutolea afya.
Amesema yale yote ambayo wanawaahidi wazee kutokana na risala yao, yatafanyiwa kazi, ikiwemo kulishawishi baraza la madiwani liweze kukubali kutenga bajeti ya kuwakatia Bima ya afya wazee wachache kwa kila mwaka ili kuwasaidia katika matibabu.
Pia ameitisha kikao cha wadau siku ya tarehe 02/10/2023 ili kujadiliana suala la kuwasaidia kuwapa Bima wazee wasiojiweza kiuchumi ikiwa ni muendelezo wa huduma ya kuwapa kadi za Bima za bure wazee, kama walivyotoa kadi za bima zaidi ya 70 bure kwa wazee tarehe 01/10/2023 ikiwa ni siku ya maadhimisho ya wazee duniani.
Aidha amewataka wataalam kuendelea kutoa elimu kwa umma juu ya imani potofu juu ya wazee, ikiwemo mzee kuhusishwa na ushirikina pale anapokuwa na macho mekundu.
"Bila wazee hata sisi tusingekuwa hapa, wazee hawa walifyatua matofali wakajenga shule wakishirikiana na serikali na ndo maana sisi leo tumesoma na tumefika hapa."
Awali Mganga Mkuu (W) Dr. Saumu Kumbisaga, amewashukuru viongozi wa baraza la wazee kwa kukubali kufanya maadhimisho ya siku ya wazee duniani, katika wilaya ya Kyela ili kuleta chachu kwa wazee wengine kutambua kuwa wazee wanatambulika katika wilaya.
Aidha amesema wilaya ya Kyela inawategemea wazee ili iweze kupiga hatua kimaendeleo.
Mwisho Mwenyekiti wa baraza la wazee Kyela ndugu Emmanuel R. Mwakalobo ametoa salamu zake kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Samia Suluhu Hassan kwa kuwakumbuka wazee katika suala la Afya.
Pia amewapongeza wataalam kutoka Ustawi wa jamii Wilaya ya Kyela, kwa kuwa karibu na wazee na kutoa msaada kwa wakati pale wanapopatwa na matatizo ya kiafya.
Mwisho
Bomani Street
Sanduku la Posta: P. O box 320 Kyela
Simu ya Mezani: 025-2540035/7
Simu ya Mkononi: 0713655466
Barua pepe: ded@kyeladc.go.tz
Haki miliki @2017 Halmashauri ya wilaya ya Kyela. Haki zote zimehifadhiwa