Wahesmiwa madiwani wa halmashauri ya wilaya Kyela, wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwapelekea fedha za kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo inafanya wilaya hiyo izidi kupaa kimaendeleo.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Katule Kingamkono, kwenye mkutano wa kawaida wa baraza la madiwani uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya wilaya ya Kyela. Kingamkono alisema wamepokea sh.bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya mama na mtoto katika hospitali ya wiaya na wanaamini fedha hizo zinakwenda kumsaidia mama ambaye alikuwa alikuwa anajifungua katika wodi ambayo haikuwa rafiki.
Alisema walipokea kiasi kingine sh.milioni 250 na baadaye kuongezewa sh.milioni 250 na hivyo kufanya jumla ya sh.milioni 500 kwa ujenzi wa kituo cha afya Itunge.Mwenyekiti wa halmashauri aliongeza kwa kusema, walipokea sh.milioni 250 kwa ujenzi wa kituo cha afya Njisi, shilingi milioni 300 za ujenzi wa kituo cha afya Kilasilo na sh.milioni 316 kwa ajili ya vifaa tiba katika hospitali ya wilaya Kyela.
"Tumepokea sh.bilioni 1.3 kutoka miradi ya Uviko-19,tumepokea fedha nyingine na mmeanza kuuona mji wetu wa Kyela katika suala la miundombinu ikiwemo ujenzi wa barabara za mitaani kwa kiwango cha lami,mji wetu sasa unaendelea kupendeza,tumpigie makofi mengi Rais Mama Samia" alisema.
Aliongeza kwa kumpongeza mbunge wa jimbo la Kyela, Ally Mlaghila maarufu Kinanasi,kwani wanaamini wanaye mbunge anayewawakilisha vyema wananchi wa wilaya hiyo.
Kingamkono alisema anaamini hayo yote yanafanyika sababu wameweza kujenga umoja na mshikamano na kwamba ana imani Kyela itaenda na wao na hivyo waendelee kuyafanya hayo.
Aidha Mhe. Kingamkono alisema yapo mambo ambayo halmashauri inaendelea kuyafanya na kumpongeza Mkurugenzi mtendaji Ezekiel Magehema, wakuu wa idara na vitengo, madiwani na maofisa watendaji wa kata kwa namna ambavyo wanaendelea kukusanya mapato.
"Mpaka robo hii tumeweza kuvuka asilimia tatu ya makIsio, tumekusanya mapato kwa asilimia 78,tunamshukuru Mkuu wa wilaya kwa usimamizi wake mzuri,tunaamini mawazo na ushauri wako unaoendelea kutoa ni sehemu ya mafanikio tuliyoyafikia" alisema Kingamkono.
Aliongeza kipekee wawapongeze maofisa watendaji wa kata kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya na kuwataka waendeleo hivyo,kwa kuhakikisha wanatimiza wajibu wao na wao (Madiwani) wanatambua jitihada zao.
"Cha msingi kwenu maofisa watendaji wa kata, ni kuendelea kufanya kazi zenu kwa kufuata misingi ya kazi, ili mambo yetu yaendelee kukaa vizuri" alisema Kingamkono.
Bomani Street
Sanduku la Posta: P. O box 320 Kyela
Simu ya Mezani: 025-2540035/7
Simu ya Mkononi: 0713655466
Barua pepe: ded@kyeladc.go.tz
Haki miliki @2017 Halmashauri ya wilaya ya Kyela. Haki zote zimehifadhiwa