Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, Adv. Florah A. Luhala, ametoa mafunzo maalum kwa watumishi wapya wa ajira mpya kwa lengo la kuwajengea uelewa kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Mafunzo hayo yalifanyika tarehe 05 Desemba 2025 katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri, ambapo watumishi hao walifundishwa masuala mbalimbali ikiwemo misingi ya utumishi wa umma, haki na wajibu wa mtumishi, misingi ya kisheria katika kusimamia haki za watumishi, pamoja na miongozo na sera zinazopaswa kuzingatiwa katika utendaji wa kazi serikalini.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Adv. Florah A. Luhala aliwataka watumishi hao kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na ufanisi, huku wakizingatia maadili ya utumishi wa umma ikiwa ni pamoja na utunzaji wa siri za serikali na taarifa za wateja wanaowahudumia katika vituo vyao vya kazi.
Aidha, aliwakumbusha kuonyesha heshima kwa viongozi, kuwahi kazini, na kufuata waraka wa mavazi unaoongoza watumishi wa umma, akibainisha kuwa hayo ni mambo muhimu katika kuimarisha taswira ya utumishi wa umma na kuhakikisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Adv. Luhala alisisitiza pia umuhimu wa kutii sheria, kanuni na taratibu zote za kiutumishi, akionya kuwa kitendo cha kwenda kinyume na miongozo hiyo kinaweza kusababisha kuchukuliwa kwa hatua za kinidhamu ikiwemo kusimamishwa kazi au kufukuzwa kulingana na makosa yatakayobainika.
Bomani Street
Sanduku la Posta: P. O box 320 Kyela
Simu ya Mezani: 025-2540035/7
Simu ya Mkononi: 0713655466
Barua pepe: ded@kyeladc.go.tz
Haki miliki @2017 Halmashauri ya wilaya ya Kyela. Haki zote zimehifadhiwa