Baraza la Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya wilaya Kyela mkoani Mbeya, limempongeza na kumshukuru Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, kwa kuboresha huduma za afya katika hospitali ya wilaya na hivyo kuwaondolea adha na kero kubwa ambayo walikuwa wanakumba nayo wananchi wilayani hapa.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya Kyela, Katule G. Kingamkono, aliyasema hayo jana tarehe 01/03/2023, wakati akitoa taarifa kuhusu masuala ya afya wilayani Kyela ikiwa ni katika kikao cha baraza la madiwani kwa robo ya pili, Kikao kilichofanyika ukumbi wa mikutano wa halmashauri uliopo Kyela mjini.
Mhe. Kingamkono alizitaja huduma zilizoboreshwa hospitalini hapo ni pamoja na vipimo vya mashine ya X-Ray ambavyo vilikuwa ni adha na kero kubwa kwa wananchi wilaya ya Kyela.
"Nitumie nafasi hii kuwapa pole wananchi wote wa wilaya ya Kyela ndani na nje, ambao walipata adha na kero kubwa wakati walipokuwa wanaenda hospitali ya wilaya kupata huduma za kitabibu" alisema Kingamkono.
Aliongeza anapenda kuwatangazia rasmi wananchi kwamba wameweka mashine ya kisasa ya X-Ray ambayo ni ya mfumo wa kompyuta tofauti na zile za zamani.
Mhe. Kingamkono alisema zamani wananchi walikuwa wanalazimika kusubiri wapigwe picha, Na kisha wasubirie waipepee picha ili ikauke ndipo iweze kusomwa taarifa zake lakini sasa hivi ni mfumo wa kompyuta ambao mgonjwa anaweza kujiangalia viungo vyake vyote vya ndani ya mwili wake.
Aidha Mwenyekiti halmashauri alisema, katika eneo la afya ya kinywa na meno,wamepata vifaa vya kisasa sasa hata huduma ya meno bandia na uzibaji wa meno yaliyotoboka sasa hivi wanao uwezo wa kusafishwa kisha kuzibwa meno yao yaliyotoboka.
Kwa upande wa chumba cha kutunzia miili ya marehemu, Kingamkono alisema wameweza kupata jokofu lenye uwezo wa kutunza miili sita kwa wakati mmoja na pia chumba kimeboreshwa na sasa kina hali bora zaidi.
"Vile vile, tumefanikiwa kununua mashine ya kisasa ya kufulia nguo ambayo kwa wakati mmoja inao uwezo wa kufua mashuka 50 ambayo itatusaidia sana katika masuala ya usafi katika hospitali yetu ya wilaya Kyela" alisema Kingamkono.
Kingamkono alilitaja eneo lingine lililoboreshwa ni chumba kwa ajili ya kufanyia mazoezi, kwa wale wanaokutwa na changamoto ya ugonjwa wa kupooza sehemu ya miili yao hivyo kwa sasa wanacho chumba maalum kwa ajili ya kufanyia mazoezi.
Bomani Street
Sanduku la Posta: P. O box 320 Kyela
Simu ya Mezani: 025-2540035/7
Simu ya Mkononi: 0713655466
Barua pepe: ded@kyeladc.go.tz
Haki miliki @2017 Halmashauri ya wilaya ya Kyela. Haki zote zimehifadhiwa