Baraza la madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya, limepitisha rasimu ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ikiwa na makisio ya shilingi bilioni 41.9 ikiwa na vipaumbele katika sekta ya afya, elimu na miundombinu ya barabara.
Akizungumza katika baraza hilo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, Katule Kingamkono alisema rasimu hiyo ya bajeti yenye makisio ya fedha kiasi cha shilingi bilioni 41.9 kitasaidia kutatua kero mbalimbali za wananchi kwa kuhakikisha vituo vya Afya, ujenzi wa vyumba vya madarasa na barabara vinakamilika.
Alisema miongoni mwa miradi inayopigiwa chapuo na bajeti hiyo ni ujenzi wa Kituo cha Afya cha Ngonga, Njisi na ukarabati wa miundombinu ya barabara na madaraja kuzunguka wilaya hiyo.
“Tunawashukuru madiwani kupitisha rasimu hii ya bajeti ambayo imesheheni masuala mbalimbali kwa maendeleo ya wilaya yetu ikiwamo matumizi ya ndani ambapo kiasi cha shilingi bilioni 4.6 kimetengwa aidha ruzuku za matumizi ya kawaida jumla ya bilioni 29, ruzuku za miradi ya maendeleo,” alisema Kingamkono.
Aidha aliwaomba wananchi kuendelea kuiunga mkono serikali katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kuwa waaminifu katika ulipaji wa kodi.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, Ezekiel Magehema wilaya hiyo inamshukuru Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia fedha nyingi kukamilisha miradi mbalimbali ikiwamo ujenzi wa Kituo cha Afya cha Itunge na ujenzi wa vyumba vya madarasa.
Aliongeza kuwa bajeti hiyo inakwenda kutimiza mahitaji ya wananchi kwa kujengewa vituo vya afya, zahanati na uboreshaji wa elimu kwa kuhakikisha mazingira ya kujifunzia na kufundishia yanaboreshwa huku wakizingatia mpango wa maendeleo kwa miaka mitano kitaifa na kimkoa sambamba na ukusanyaji wa mapato alisema Magehema.
Aidha aliongeza kuwa Wilaya hiyo imejipanga vyema kukusanya mapato na kuvuka lengo la mwaka jana ambapo walikusanya asilimia 104 mwaka 2021/2022 na kwa hadi sasa wamefanikiwa kukusanya asilimia 53 na lengo ni kukusanya zaidi ya asilimia 100.
Alibainisha mgawanyo wa fedha za ruzuku kutoka serikali kuu kuwa ni Elimu ya Msingi kimetengwa kiasi cha shilingi milioni 631. Elimu sekondari 605, ardhi na maliasili milioni tatu.
Baadhi ya madiwani akiwamo wa viti maalum, Tumain Mwakatika alisema bajeti hiyo imegusia asilimia 10 ya wanawake na vijana na kwamba kupitia fedha hizo jitihada za wananchi kujikwamua na umasikini zitaongeza.
Bomani Street
Sanduku la Posta: P. O box 320 Kyela
Simu ya Mezani: 025-2540035/7
Simu ya Mkononi: 0713655466
Barua pepe: ded@kyeladc.go.tz
Haki miliki @2017 Halmashauri ya wilaya ya Kyela. Haki zote zimehifadhiwa