Watumishi 9 wa Halmashauri ya wilaya Kyela, mkoani Mbeya wamefukuzwa kazi, baada ya kushindwa kurejesha fedha za makusanyo ya mapato,walizokuwa wamezikusanya lakini hawakuziingiza katika akaunti ya halmashauri kwa miaka mingi.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya kufanyika kwa vikao vyote vya kisheria, na watumimishi hao wote wamebainika kwa makosa ya wizi, wa kukusanya fedha za umma pasipo kuziingiza katika akaunti ya halmashauri ambalo ni kosa la kisheria.
Aidha Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya Kyela, Mheshimiwa Katule Kingamkono, alitoa maamuzi hayo tarehe 05/11/2022 mara baada ya baraza la madiwani, lililokuwa likiendelea katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo kujigeuza kuwa kamati ili kuweza kufikia maamuzi kuhusu suala hilo la muda mrefu.
Mheshimiwa Kingamkono alisema pale mtumishi wa umma anapokwenda kinyume na majukumu yake ikiwa ni uwajibikaji, masuala ya wizi ama kutumia nafasi yake vibaya, basi baraza la madiwani pia limepewa mamlaka kwa kutumia taratibu, sheria na kanuni za utumishi kuwashughulikia watumishi kwa kufuata taratibu hizo.
Aliongeza kwa kusema maamuzi haya yamefanyika baada ya Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri, Ndugu Ezekiel Magehema na wataalaam kufanya michakato yao, Na baraza kutoa maelekezo ya kufanyika kwa mchakato huo ndani ya siku tisini, ambazo zipo kwa mujibu wa sheria.
Alisema fedha hizo zilitakiwa kuleta maendeleo kwa wananchi wa Kyela, lakini wakawa wanasubiri siku za kisheria zifike, kwa hiyo wanapenda kutoa taarifa kwa umma, kwamba yale ambayo walimuagiza mkurugenzi sasa taratibu zimekamilika.
Mheshimiwa Kingamkono alisema, vikao vyote vya kisheria vimetumika kutoa maamuzi hayo, kwa hiyo anatoa taarifa kwamba wale wote ambao wamebainika kwa makosa ya wizi, wa kukusanya fedha za umma pasipo kuziingiza katika akaunti ya halmashauri lazima waondolewe kazini.
“Kwa hiyo leo baraza la madiwani kwa mamlaka lililopewa, kwa vifungu ambavyo vimeanishwa katika kanuni za serikali za mitaa, namna ya kuendesha kwa hiyo tunao watumishi tisa ambao tumewafuta kazi” Alisema Mhe. Kingamkono.
Aliongeza kwa kusema, wataendelea kuchukua hatua za kisheria, pasipo kumuonea mtu sababu hao wanaowafuta kazi, hakuna aliyeonewa na kuwa ni aibu sana leo yupo mwananchi asipotoa michango anachukuliwa hatua, wengine wanapelekwa mahakamani, wanalipa adhabu, kisha watumishi wengine wanazitumia pesa hizo kinyume na taratibu, Baraza la Waheshimiwa madiwani kamwe haliwezi kuendelea kucheka na watu, ambao wamekusanya fedha za umma, na kuzila wakati fedha hizo zingeenda kuchochea zaidi maendeleo ndani ya halmashauri ya wilaya ya Kyela.
Mwisho…….
Bomani Street
Sanduku la Posta: P. O box 320 Kyela
Simu ya Mezani: 025-2540035/7
Simu ya Mkononi: 0713655466
Barua pepe: ded@kyeladc.go.tz
Haki miliki @2017 Halmashauri ya wilaya ya Kyela. Haki zote zimehifadhiwa