Mkuu wa wilaya ya Kyela Mheshimiwa Josephine Keenja Manase amekemea vikali vitendo vibaya vinanavyoendelea kufanyika katika jamii yetu, hasa vitendo vya Ushoga, Ulawiti na Ukatili dhidi ya wanawake.
Mheshimiwa mkuu wa wilaya amekemea vitendo hivyo wakati akifungua mafunzo Elekezi, kwa wajumbe wa Baraza la Mamlaka ya Mji Mdogo wa Kyela, mafunzo yaliyofanyika tarehe 06/04/2023, katika ukumbi wa mikutano wa Mamlaka hiyo.
"Viongozi Tuwe mstari wa Mbele katika kutoa taarifa kwenye vyombo husika punde tunapoona au kusikia, mwananchi yeyote anafanyiwa vitendo hivyo ili tuweze kujenga kizazi chenye misingi na maadili mema katika jamii" amesema Mhe. Josephine Manase.
Hata hivyo Mheshimiwa Mkuu wa wilaya, amewataka viongozi hao kuwa mstari wa mbele katika kusimamia maadili katika jamii, kwa kukemea vitendo vyote viovu vinavyofanyika kinyuma na mila zetu za kiafrika.
Aidha Mheshimiwa Manase ametoa pongezi nyingi kwa wajumbe wa baraza hilo, ambao wamekuwa wakichapa kazi nzuri za usimamizi wa shughuli za maendeleo, na kuhakikisha kwamba sisi sote hatuwezi kumwangusha Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa jitihada zake anazotufanyia wana Kyela hasa katika kutuletea maendeleo.
Amesema kazi zote zinazofanywa na baraza hilo, zinaonekana na viongozi wanaziona, ameongeza kusema, viongozi wote hapa wilayani Kyela wataendelea kutoa ushirikiano kwa baraza hilo, kadri watakavyoweza ili kuleta maendeleo kwa wilaya yetu.
Pamoja na hayo, Mhe. Mkuu wa wilaya ametoa shukrani zake za dhati kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuikumbuka wilaya yetu ya Kyela, Na kutuletea miradi mingi ya maendeleo ikiwemo miradi ya ujenzi wa zahati, vituo vya afya, shule na miradi mingine mingi.
"Tutaendelea kuipeperusha bendera ya Chama Cha Mapinduzi, na tutaendelea kuupiga mwingi sababu tupo ndani ya Chama Cha Mapinduzi na tunatekeleza Ilani ya Chama chetu" amesema Mhe. Josephine Manase.
Kwa upande wa mikopo ya 10% inayotolewa kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, Mheshimiwa Mkuu wa wilaya amewataka viongozi hao kwenda kutoa elimu juu ya urejeshaji wa mikopo kwa vikundi vyote, ambavyo vimenufaika na mikopo hiyo kwa wilaya ya Kyela.
"Naomba sana viongozi msiwapitishie mikopo vikundi vyote ambavyo vina wanachama wasiotoka katika eneo lako la kiutawala" amesema Mhe. Mkuu wa wilaya.
Awali, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Mamlaka ya Mji Mdogo wa Kyela, Mheshimiwa Michael Mwakibinga alitoa pongezi kwa wajumbe hao, katika suala la kufanya kazi kwa jitihada kubwa ya kuwaletea maendeleo wananchi wa wilaya ya Kyela pamoja na ukusanyaji mzuri wa mapato.
Mwisho.
Bomani Street
Sanduku la Posta: P. O box 320 Kyela
Simu ya Mezani: 025-2540035/7
Simu ya Mkononi: 0713655466
Barua pepe: ded@kyeladc.go.tz
Haki miliki @2017 Halmashauri ya wilaya ya Kyela. Haki zote zimehifadhiwa