MKUU wa wilaya Kyela, mkoani Mbeya, Josephine Manase, amesema ameridhishwa na usimamizi wa madiwani, katika miradi ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa kwa kasi wilayani hapa.
Amesema madiwani kwa kushirikiana na safu nzima ya uongozi wa halmashauri ya wilaya, wameendelea kuifuatilia kwa umakini miradi na yeye ametembelea baadhi ya miradi na kuiona ipo katika viwango sahihi.
Mhe. Josephine aliyasema hayo juzi tarehe 01/03/2023, wakati akitoa salaam zake, katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika ukumbi wa mikutano wa halmashauri.
“Pamoja na kazi nzuri mnazoendelea kuzifanya, naomba nitilie msisitizo katika baadhi ya mambo ambayo nitaomba msaada wenu, kwa ajili ya kwenda kuyatekeleza katika maeneo yenu” alisema Josephine.
Kuhusiana na suala la elimu Mhe. Josephine alisema jambo la kwanza analosisitiza ni kuhusu watoto wote waliofaulu, kujiunga kidato cha kwanza waweze kwenda shule, na hilo liwe ni jukumu la kila mmoja lisiwe linaachwa utekelezwaji wake kwa serikali peke yake.
Alisema kama kuna sehemu kuna changamoto, labda mzazi hataki kumpeleka mtoto shule, wapeane taarifa ili waweze kuelekezana nini cha kufanya ili watoto waweze kupata elimu.
“Kama mnavyojua Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, anatoa elimu bure hakuna ada, kinachotakiwa ni mtoto kwenda shule tu, tuwasisistize sababu elimu wanayoipata itakuja kumsaidia siyo mtoto tu, bali hata wazazi wake na taifa kwa jumla” alisema Josephine.
Kwa upande wa mapato Mhe. Mkuu wa wilaya alisema halmashauri inategemea mapato inayokusanya ili kuleta maendeleo katika wilaya hiyo, na kwamba ukusanyaji wake ni mzuri lakini anaomba waendelee kupeana elimu ya namna ya kutumia mashine za kukusanyia.
Amekiri kuwa na changamoto chache, lakini wajaribu kuendelea kupeana elimu ili watu waendelee kuzitumia mashine sababu ndizo zinawasaidia wao kukusanya mapato, na kupata kwao mapato ndipo kunapelekea mapato hayo baadaye yataenda kuwasaidia katika kurekebisha barabara zao na huduma nyingine mbalimbali.
“Naomba tupeane elimu juu ya ukusanyaji wa mapato, liwe ni jukumu la kila mmoja wetu ili kuwapa watu elimu sahihi juu ya mapato” alisema Josephine.
Kwa upande wa ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo Mhe. Josephine alisema pamoja na kwamba amepongeza miradi inayotekelezwa kuendelea vyema, anaomba pia waendelee kuwa mabalozi na mawakili katika kufuatilia miradio hiyo, ili kuhakikisha inatekelezwa kulingana na muda uliowekwa, lakini kwa ubora unaotakiwa.
Alisema vituo vya afya vikijengwa katika ubora, basio vitakaa kwa muda mrefu na watakuwa wanaokoa gharama za serikali katika kurekebisha miradi hiyo, badala ya kutenga fedha kwa ajili ya kufanya shughuli nyingine.
“Kwa hiyo naomba tuwe mabalozi, lakini pia tuwe mawakili wa kuhakikisha ile miradi inakamilika kwa wakati lakini pia kuhakikisha inakuwa na viwango vinavyotakiwa, kama mradi upo chini ya kiwango na wewe umepitia na kuiona kasoro hiyo, ni vyema tupeane taarifa…” alisema Mhe. Manase.
Pamoja na hayo Mhe. Josephine alisema mvua zimeanza na wanatambua kuna sehemu ambazo huwa zinaathirika na mafuriko, anawaomba wachukue tahadhari lakini pia wawaelemishe wananchi juu ya namna bora ya kujikinga na mafuriko.
Aliwataka wapeane ushirikiano katika kuhakikisha kila mwananchi anakuwa salama wilayani.
Hata hivyo Mheshimiwa Josephine alisema kama kuna changamoto yoyote, katika masuala ya pembejeo ni vyema wapeane taarifa na hasa ukichukulia wilaya yetu ina mazao ya kibiashara, ambayo ndiyo yanayotubeba katika uchumi watu.
Alisema hivyo mazao hayo yakishindwa kuwa bora , sababu ya ukosefu wa pembejeo kama kuna changamoto sehemu, serikali ya Rais Dk.Mama Samia ni sikivu hivyo wapeane ushauri, taarifa kama kuna changamoto yoyote.
Aidha katika suala la usafi wa mazinhira, Mheshimiwa, Alisema nchi jirani (Malawi), wanasumbuliwa na ugonjwa kipindupindu hivyo ni vyema waweke mazingira safi kwani ugonjwa huo kuingia wilayani humu ni suala la dakika moja tu, hivyo tusipoweka mazingira safi ina maana tunajihatarisha sisi wenyewe.
Bomani Street
Sanduku la Posta: P. O box 320 Kyela
Simu ya Mezani: 025-2540035/7
Simu ya Mkononi: 0713655466
Barua pepe: ded@kyeladc.go.tz
Haki miliki @2017 Halmashauri ya wilaya ya Kyela. Haki zote zimehifadhiwa