Mkuu wa Wilaya ya Kyela Mhe. Josphine Manase amefanya ziara ya kusikiliza na kutatua kero za Wananchi katika vijiji vya Masebe One na Bwato leo tarehe 15.07.2025, ambapo ametoa maelekezo na ushauri mbalimbali kwa maendeleo ya Vijiji vya Masebe one na Bwato Pamoja na Kyela kwa ujumla.
Akizungumza katika Ziara hiyo Mkuu wa Wilaya ya Kyela amewahimiza vijana kuchangamkia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, ili waweze kubuni biashara mbalimbali zitakazowasaidia kujikwamua kiuchumi na kuboresha maisha yao.
Aidha DC Manase amewahamasisha vijana kuendelea kujituma na kujiimarisha kimichezo kwa kujenga timu katika ngazi ya vijiji, ili baadaye zipatikane timu bora zitakazoiwakilisha Wilaya katika mashindano mbalimbali. Amesema kuwa viwanja vipo na fursa zipo, hivyo kinachotakiwa ni juhudi, nidhamu na mshikamano miongoni mwa vijana.
Mkuu wa Wilaya ya Kyela ameahidi kulifanyia kazi suala la kutokuwajibika kwa watoa huduma katika Kituo cha Afya cha Ipinda. Amewataka watoa huduma wote wa afya kuwajibika ipasavyo katika nafasi zao na kuacha mara moja tabia ya kuwakwamisha wananchi kupata huduma stahiki. Amesisitiza kuwa Serikali haivumilii uzembe au utovu wa maadili katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela Adv.Florah A. Luhala akijibu kero Kuhusiana na kupanda na kushuka kwa bei ya zao la kakao, Mkurugenzi ameeleza kuwa zao hilo kwa sasa lipo katika mfumo rasmi wa TMX ambapo wanunuzi huongozwa na soko la dunia.
Pia amewashauri wakulima kutunza kakao vizuri na kuacha tabia ya kuuza kakao mbichi kwani inaharibu sifa ya kakao ya Kyela inayotambulika kimataifa.
Mkurugenzi amehimiza wazazi kuhakikisha kuwa watoto wote waliotimiza umri wa kuanza shule hawakai nyumbani kwa shughuli nyingine, bali waandikishwe na wahudhurie masomo kama inavyotakiwa kisheria na kwa manufaa ya maisha yao ya baadaye.
Mkurugenzi amewahimiza wananchi wote kushirikiana na Serikali katika kulinda heshima ya kakao ya Kyela na kuifanya kuendelea kuwa bora duniani.
Bomani Street
Sanduku la Posta: P. O box 320 Kyela
Simu ya Mezani: 025-2540035/7
Simu ya Mkononi: 0713655466
Barua pepe: ded@kyeladc.go.tz
Haki miliki @2017 Halmashauri ya wilaya ya Kyela. Haki zote zimehifadhiwa