Kamati ya siasa ya Mkoa wa Mbeya ikiongozwa na mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa, Mhe. Dkt. Steven Mwakajumilo imetembelea na kukagua miradi ya maendeleo hapa wilayani Kyela leo tarehe 11/03/2023.
Akiongea katika ziara hiyo, Mheshimiwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mbeya mesema,
Kamati ya siasa inapokuja kukagua na kutembelea miradi si lazima wakague miradi waliyopangiwa, bali wanauwezo wa kukagua mradi wowote wa maendeleo ili kujiridhisha na utekelezaji wake.
Miradi iliyotembelewa na kukaguliwa ni pamoja na mradi wa Ujenzi wa bweni la wasichana katika shule ya sekondari Nyasalakeshore, Kikundi cha Umoja cha watu wenye ulemavu kilichonunua boti ya uvuvi katika kata ya Matema, Mradi wa ujenzi wa kituo cha afya kata ya Makwale pamoja na ujenzi wa daraja katika kata ya Mababu.
Aidha Mhe. Mwenyekiti ametoa pongezi kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kyela, Ndugu Ezekiel H. Magehema kwa kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, kwani ametoa mikopo kwa vikundi vya Wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kama ilani ya Chama inavyotamka.
"Mikopo hii si sadaka ni mikopo ambayo inatengwa ili iweze kujizungusha. Hivyo kikundi chochote kinachopata mkopo ni lazima kiweze kurejesha mkopo huo ili uweze kusaidia wengine" amesema Mhe. Mwakajumilo.
Ameiagiza Halmashauri kuwa na taarifa ya vikundi vyote vilivyokopeshwa ikiwa ni pamoja na kuwa na taarifa ya shughuli zinazotekelezwa na vikundi hivyo.
Pamoja na hayo Mhe. mwenyekiti alisema tunazo meli ambazo zinaweza kutusaidia katika shughuli za kufungua biashara zetu hata katika nchi jirani kama tutazitumia vizuri.
Katika kilimo Mhe. Mwakajumilo, ameitaka Halmashauri ya wilaya ya Kyela, kuanzisha uvuvi wa vizimba vya samaki, ili wilaya ya Kyela ipate mazao mapya yatakayoiletea mapato wilaya ya Kyela.
Kwa upande wa wawatumishi, Mheshimiwa Mwenyekiti, amewataka wataalam kubadilika na kuto fanya kazi kwa mazoea. Pia amewataka kutoka ofisini na kwenda kuwatumikia wananchi.
Kwa upande wa Elimu amesema, amepata faraja kuona mchango wake wa shilingi milioni 1 haujapotea kwani Bweni la shule ya Nyasa lakeshore limejengwa.
Pia amesema mbali na kujenga, mabweni amewataka wazazi kubadilika katika malezi ya watoto na sio kuwaachia wafanyakazi wa ndani kuwalea watoto.
Hata hivyo Mhe. Mwakajumilo amesema, Wanafunzi wengi kutoka wilaya ya Kyela watashindwa kujiunga na kidato cha tano kwa sababu wilaya ya Kyela inazo shule chache za kidato cha tano.
Hivyo ameitaka Halmashauri kuweka mpango wa kujenga shule za kidato cha tano.
Aidha Mheshimiwa Mwenyekiti wa Chama Tawala Mkoa, amekemea tabia ya kuwaruhusu wanafunzi kusoma hadi saa nne usiku kisha kurudi majumbani mwao, amekataza utaratibu huo kwani ni hatarishi kwa usalama wa wanafunzi hao.
Nae katibu wa vijana wa Chama cha Mapinduzi Mkoa ndugu Yusufu Mabena, alishauri kuwa wanafunzi wanaosoma usiku wapunguziwe muda wa kutoka usiku, kutokana na usalama wa wanafunzi wao.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya Mhe. Elias Mwanjara ametoa pongezi kwa mikopo inayotolewa na Halmashauri hadi kuviwezesha vikundi kuanzisha mitaji mbalimbali na kubadili maisha ya wanavikundi hao na wananchi.
Ziara hiyo itaendelea tarehe 12/03/2023.
Bomani Street
Sanduku la Posta: P. O box 320 Kyela
Simu ya Mezani: 025-2540035/7
Simu ya Mkononi: 0713655466
Barua pepe: ded@kyeladc.go.tz
Haki miliki @2017 Halmashauri ya wilaya ya Kyela. Haki zote zimehifadhiwa