Mkuu wa wilaya ya Kyela Mhe. Josephine Manase ametembelea kijiji cha Njugiro kata ya Ipande, akiendelea na ziara yake ya kusikiliza kero mbalimbali zinazo wakabili wananchi katika wilaya ya Kyela.
Katika ziara hiyo iliyofanyika tarehe 05/07/2024, Mkuu wa wilaya ya Kyela Mhe. Josephine Manase amefurahishwa na wananchi, kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kutoa kero zao.
Mhe. Mkuu wa wilaya ya Kyela, amefanikiwa kutoa suluhisho ya kero zilizokuwa zinawakabili wananchi wa kata ya Ipande, ambapo wananchi walitoa kero mbalimbali zinazowasumbua ikiwemo suala la afya, Elimu, Kilimo pamoja na Umeme.
Kuhusu suala la ukosefu wa zahanati, Mhe. Josephine Manase ameahidi kutoa kiasi cha Tsh. 200,000 kama chachu, kwaajili ya kuhamasisha mchakato wa kuanza ujenzi wa zahanati katika kijiji hicho cha Njugiro.
Suala la umeme kupatikana maeneo ya masoko, na shuleni katika kijiji hicho, Mratibu wa umeme wa "REA" Ndugu. Jairo Simion Sichura amewatoa hofu wakazi wakijiji hicho cha Njugiro kuwa katika mwaka mpya wa fedha Serikali imetenga bajeti kubwa ambapo mpaka kufikia mwakani vijiji vingi vitapata umeme na kijiji cha Njugiro kitapewa kipaumbele.
Pamoja na hayo Mkuu wa wilaya ya Kyela ameumizwa na ukosefu wa daraja lililosombwa na maji, daraja ambalo lilikuwa lina unganisha kitongoji cha Kipela na Njugiro ambapo limeleta adha ya mawasiliano baina ya vitongoji hivyo viwili, pia limesababisha kukosekana kwa baadhi ya huduma za kijamii.
Aidha Mkuu wa wilaya ya Kyela Mhe. Josephine Manase amewaahidi wananchi hao kuwa, anaenda kulifanyia kazi suala hilo na atarudi na suluhisho mara moja.
"Kumekua na mazoea mabaya ya vijana wa Bodaboda kuendesha Pikipiki mpaka kwenye Madaraja ya kamba (viteputepu) ambapo wanaharibu mbao za madaraja hayo" alisema Mhe. Josephine Manase.
Kwa upande wa Mkuu wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Kyela (OCD) Ndug. Lwitiko Mwanjala amewaasa vijana wa Bodaboda kuzingatia sheria za barabarani kwa manufaa yao wenyewe na familia zao.
Mwisho Mhe. Josephine Manase amehitimisha ziara hiyo kwa kuwataka wananchi wa kata ya Ipande kutumia haki yao ya kikatiba kuchagua viongozi bora kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa. Pamoja na kushirikiana katika kupiga vita mimba za utotoni.
Bomani Street
Sanduku la Posta: P. O box 320 Kyela
Simu ya Mezani: 025-2540035/7
Simu ya Mkononi: 0713655466
Barua pepe: ded@kyeladc.go.tz
Haki miliki @2017 Halmashauri ya wilaya ya Kyela. Haki zote zimehifadhiwa