Mkuu wa wilaya ya Kyela Mheshimiwa Josephine Manase amemtaka Meneja wa Maji RUWASA wilayani Kyela, kutoa taarifa ya wadaiwa wa madeni ya maji na waliolipa madeni ya maji, ndani ya siku 60.
Mhe. Mkuu wa wilaya, ameyasema hayo wakati akitoa hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano mkuu wa nusu mwaka wa vyombo vya watoa huduma ya maji ngazi ya jamii "CBWSOs", mkutano uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa chuo cha ufundi KPC tarehe 17/10/2023.
Aidha amesema, anafarijika kuona RUWASA tangu ianze kazi rasmi Julai 2019, kwa wilaya ya Kyela, imepata mafanikio ikiwemo kuongeza asilimia ya wanaopata huduma ya maji kutoka 68% hadi 70.24%.
Ambapo ni pamoja na kurudisha huduma ya maji kwenye maeneo kama Kitongoji cha Lyulilo katika Kijiji cha Ikombe, kukarabati miradi ya Matema na ikombe.
"Ndugu Wajumbe wa Mkutano, hadi sasa najua miradi ya maji inaendelea kujengwa ambapo itapandisha asilimia ya upatikanaji wa huduma kutoka 70.24% ya sasa hadi 86% hapo Juni 2025, yaani Lema itaongeza 2%, Ngana 9% na Sinyanga 5%". amesema Mhe. Mkuu wa wilaya.
Aidha amezitaja gharama za mradi wa Ngana group kuwa ni Shilingi 6,779,238,735.00, mradi wa Lema shilingi 490,219,018.54 na mradi wa Sinyanga group shilingi 814,784,250 fedha zilizotolewa na Mheshimwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan kwenye sekta ya maji katika wilaya ya Kyela.
Kwa niaba ya wananchi wa wilaya ya Kyela, Mhe. Mkuu wa wilaya amemshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa fedha za miradi na kuahidi kuzisimamia ili kuhakikisha zinatatua kero ya maji kwa wananchi wa Kyela.
Pia amewataka viongozi wote wilayani kusaidiana katika kutoa elimu juu ya utunzaji wa vyanzo vya maji.
Awali Meneja wa maji(W) Eng. Deule alisema ipo mipango mizuri ambayo RUWASA Kyela imejipanga kuinua huduma za maji kwa mwaka 2023/2024, akaitaja mipango hiyo kuwa ni ;
Kufanya maandalizi ya mradi mkubwa wa maji utakaotumia ziwa Nyasa kama chanzo chake cha maji, kuendelea na awamu ya 2 ya Maboresha ya mradi wa maji wa Sinyanga group ya usambazaji wa maji na ujenzi wa chujio, kuendelea na ukamilishaji wa Ujenzi wa mradi wa maji wa Ngana group utakaohudumia vijiji 25.
Pamoja na hayo mipango mingine ni kuendelea na ujenzi wa mradi wa maji kwa kijiji cha Lema, kukarabati bomba kuu la mradi wa maji wa Ngamanga group, kukarabati mradi wa maji wa Makwale, kuboresha miradi ya maji ya Masoko, Busoka na Lubaga kwa kufunga nishati ya umeme jua.
Eng. Deule amesema mipango mingine ni kukarabati skimu ya Maji ya Ngyekye, kujenga madakio ya miradi wa maji wa Matema na Ikombe, kuunda chombo cha watoa huduma ya maji ngazi ya jamii (CBWSO) cha Ngana na kufanya usanifu wa Mradi wa Maji wa Busale group utakaohudumia vijiji vya kata ya Busale
Mwisho.
Bomani Street
Sanduku la Posta: P. O box 320 Kyela
Simu ya Mezani: 025-2540035/7
Simu ya Mkononi: 0713655466
Barua pepe: ded@kyeladc.go.tz
Haki miliki @2017 Halmashauri ya wilaya ya Kyela. Haki zote zimehifadhiwa