Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Zuber Homera amezitaka Halmashauri za Mkoa wa Mbeya kuweka kipaumbele cha utoaji wa mikopo kwa wananchi ambao wamejikita katika kuanzisha viwanda vya uzalishaji wa bidhaa.
Ameyasema haya wakati wa hafla fupi ya kukabidhi mashine za usindikaji wa bidha zitokanazo na zao la kakao, mashine zilizokabidhiwa kwa mabinti walio katika mpango wa DREAMS uliopo chini ya shirika la HJFMRI, Hafla hiyo imefanyika katika viwanja vya ukumbi wa Halmashauri hapa wilayani Kyela.
Akizungumza kabla ya kukabidhi mashine hizo Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa amesema, anaziagiza Halmashauri za Mkoa wa Mbeya kuanza kutoa vipaumbele vya kutoa mikopo kwa vikundi vya wananchi ambao wamejikita katika kuanzisha viwanda vya uzalishaji. Kwani mkoa wetu kwa sasa unahitaji mabadiliko ya kiuchumi hivyo hatupaswi kugawana pesa hizi za mikopo kama njugu bali tutoe mikopo yenye tija.
Aidha Mheshimiwa Homera alimuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kyela Ndugu Ezekiel H. Magehema kutoa mkopo kwa kikundi cha mabinti ambao wamekabidhiwa mashine, ili kuweka alama ya maendeleo ambayo haitakuja kufutika maishani na hasa kwa kipindi hiki ambacho wilaya ya Kyela imekuwa mstari wa mbele katika suala la maendeleo.
"Magehema ukitaka kutoa mkopo kwa hawa mabinti usisite kwani mabinti hawa ni miongoni mwa vijana waadilifu na waaminifu sana" alisema Mhe. Homera.
Nae Mbunge wa jimbo la Kyela Mheshimiwa Ally Mlaghila Jumbe amesema, Halmashauri ya wilaya ya Kyela kwa kushirikiana na viongozi wote wa wilaya, wataendelea kuwasimamia mabinti hao na kuzitunza mashine na kuhakikisha mashine hzo, zinakwenda kubadili Maisha ya mabinti hao ambao wametolewa katika mazingira hatarishi na kwa sasa wameanza kuona mwanga bora wa Maisha yao.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kyela Mheshimiwa Katule G. Kingamkono alisema, kwa niaba ya Baraza la Waheshimiwa Madiwani wa wilaya ya Kyela, watakwenda kuwasimamia mabinti hao na kuwafanya kuwa kielelezo cha maendeleo katika wilaya. Pia aliwaasa vijana hao kupendana na kuwa na ushirikiano baina yao ili kuleta matunda katika kazi watakazokuwa wanazifanya kwa umoja wao.
Akisoma taarifa kwa mgeni rasmi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kyela Ndugu Ezekiel H. Magehema amesema,
Halmashauri ya wilaya ya Kyela kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya imekwisha ainisha eneo lenye ukubwa wa hekari 17, kwa ajiri ya shamba la kakao katika eneo la kata ya Talatala na pia imetenga eneo katika kata ya Kajunjumele kwa ajiri ya ufungaji wa mashine hiyo.
Pamoja na hayo Ndugu Magehema amesema, Halmashauri ya wilaya ya Kyela haipo nyuma kimaendeleo kwani imeweza kutoa mkopo kwa vikundi viwili mkopo wenye thamani ya shilingi 8,000,000/= kwa mwaka huu wa fedha. Hii ni kwa ajiri ya kuinua Maisha ya vijana, lakini Halmashauri imetenga shilingi milioni 124 kwa kusudi la kuwakopesha vijana Zaidi.
Mwisho viongozi wote walitoa pongezi zao za dhati kwa shirika la HJFMRI kwa ufadhiri wa mshine za usindikaji wa zao la kakao mashine zenye thamani ya shilingi 40,828,00/=. Ambazo zitakuwa ni chachu ya maendeleo kwa wilaya ya Kyela, kwani zitaongeza soko la uhakika la zao la kakao hapa wilayani, na kutoa ajira Zaidi ya kaya 200 ambapo bidhaa kama cocoa batter, mafuta ya kakao na unga wa kakao utatengenezwa na kupatikana hapahapa wilayani.
Mwisho.
Bomani Street
Sanduku la Posta: P. O box 320 Kyela
Simu ya Mezani: 025-2540035/7
Simu ya Mkononi: 0713655466
Barua pepe: ded@kyeladc.go.tz
Haki miliki @2017 Halmashauri ya wilaya ya Kyela. Haki zote zimehifadhiwa