Mkuu wa mkoa wa Mbeya Mheshimiwa Juma Zuberi Homera, leo tarehe 10/10/2023, amekagua miradi ya maendeleo ikiwemo mradi wa ujenzi wa vyumba 2 vya madarasa na matundu 3 ya vyoo katika shule ya msingi Mababu, ujenzi wa vyumba 2 vya madarasa na matundu 3 ya vyoo katika shule ya msingi Mapinduzi kata ya Makwale, skimu ya umwagiliaji Makwale na kisha kumaliza ziara yake kwa kufanya mkutano wa hadhara katika kata ya Ngonga ili kusikiliza kero za wananchi.
Akiongea na wananchi wa kata ya Ngonga Mkuu wa mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Zuberi Homera, amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kyela, kumalizia jengo la maabara ndani ya siku 60, jengo linalojengwa katika kituo cha afya Ngonga.
Kuhusiana na kero ya barabara katika kata ya Ngonga Mhe. Homera, amewataka wataalamu wa TARURA, kufanya tathimini na kujua gharama ya ulimaji wa barabara katika kata ya Ngonga na andiko hilo lifike Ofisini kwake, ili alifanyie kazi, ila amewataka wataalamu hao, kuto andika gharama kubwa za ujenzi ambazo zinaweza leta ugumu katika utekelezaji wake.
Pamoja na hayo katika suala la umeme, Mhe. Mkuu wa mkoa amelitaka shirika la umeme wilaya ya Kyela kuorodhesha vitongoji vyote vilivyopo katika kata ya Ngonga, ambavyo havina umeme, na ambavyo havimo katika mpango wa kupata umeme kwa mwaka huu, ili aweze kuviombea bajeti kwa Mhe. Rais kwa mwaka huu, na kuvikamilisha kwa huduma ya umeme, amesema, anaamini jambo hilo litatekelezeka.
Aidha amemtaka mkandarasi anaeshughulikia mradi wa usambazaji wa maji hadi kata ya Ngonga, kukamilisha mradi huo hadi ifikapo tarehe 30/12/2023, ili wananchi wa Ngonga waweze kupata maji safi na salama.
Kuhusiana na suala la changamoto ya masoko ya matikiti, amemuagiza afisa kilimo wa wilaya kufanya tathimini ya idadi ya matikiti yaliyozalishwa ndani ya wilaya, ili kuyatafutia masoko nje ya wilaya ya Kyela.
Katika suala la kilimo, Mhe. Homera amesema, mbolea zitapatikana katika kata kwa kupitia chama cha msingi na amemtaka mtendaji wa kata kubandika bei za mbolea mbalimbali katika kata, ili kila mwananchi ajue aina na bei ya mbolea.
Pia Mhe. Mkuu wa mkoa amechangia shilingi milioni 1 katika ujenzi wa bweni katika shule ya sekondari Ngonga, shilingi laki 5 kwa walimu wanaojitolea na kufanya vizuri na shilingi laki 5 kwa watumishi wa Afya wanaofanya kazi kwa bidii.
Mwisho aliwahakikishia wananchi kwamba Serikali ipo macho na itaendelea kutatua changamoto zote za wananchi.
Bomani Street
Sanduku la Posta: P. O box 320 Kyela
Simu ya Mezani: 025-2540035/7
Simu ya Mkononi: 0713655466
Barua pepe: ded@kyeladc.go.tz
Haki miliki @2017 Halmashauri ya wilaya ya Kyela. Haki zote zimehifadhiwa