MKUU WA WILAYA KYELA AONGOZA TATHMINI YA MICHEZO YA UMITASHUMTA NA UMISSETA.
Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Mhe. Josephene Manase, ameongoza tafrija ya tathmini ya michezo ya UMITASHUMTA na UMISSETA iliyofanyika tarehe 15 Agosti 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Manase aliwapongeza walimu kwa kujitoa kwa hali na mali kuhakikisha wanafunzi wanashiriki michezo bila kuathiri ratiba zao za masomo. Alisema jitihada hizo zinaonyesha dhamira ya dhati ya kukuza vipaji vya michezo mashuleni.
Aidha, Mkuu wa Wilaya alitumia nafasi hiyo kumpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kyela, Adv. Florah A. Luhala, kwa kutoa hamasa kubwa kwa walimu na wanafunzi. Alisema uongozi wa Adv. Luhala umekuwa mstari wa mbele kuwashika mkono walimu na wanafunzi katika kuhakikisha Wilaya ya Kyela inapiga hatua kubwa kwenye michezo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kyela, Adv. Florah A. Luhala, ameahidi kuendelea kushirikiana na walimu na wadau wote ili kuhakikisha Kyela inaendelea kung’ara kimichezo katika Mkoa wa Mbeya na taifa kwa ujumla.
Aidha, Adv. Luhala aliwashukuru wadau mbalimbali wanaounga mkono juhudi za kukuza michezo mashuleni, akisema msaada wao umekuwa chachu ya mafanikio ya Kyela katika mashindano haya na ni mfano wa mshikamano wa jamii kwa maendeleo ya elimu na michezo.
Hafla hiyo pia ilihusisha ugawaji wa vyeti na zawadi kwa shule pamoja na tarafa zilizofanya vizuri zaidi katika mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA mwaka huu. Tuzo hizo zilitolewa kama ishara ya kutambua na kuthamini jitihada za wachezaji, walimu na viongozi wa michezo.
Bomani Street
Sanduku la Posta: P. O box 320 Kyela
Simu ya Mezani: 025-2540035/7
Simu ya Mkononi: 0713655466
Barua pepe: ded@kyeladc.go.tz
Haki miliki @2017 Halmashauri ya wilaya ya Kyela. Haki zote zimehifadhiwa