Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Arthur Nanauka, ameendelea na ziara yake ya kusikiliza na kutatua kero zinazowakabili vijana katika Wilaya ya Kyela tarehe 27 Novemba 2025.
Akizungumza na vijana wa wilaya hiyo, Mhe. Nanauka alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutambua nafasi na mchango mkubwa wa vijana katika maendeleo ya Taifa. Amesema uamuzi wa Rais kuunda Wizara maalum ya Maendeleo ya Vijana ni hatua muhimu inayolenga kuwawezesha vijana na kujenga Taifa lenye nguvu na dira ya maendeleo.
Aidha, Mhe. Waziri amesisitiza kuwa vijana ni wadau wakubwa wa maendeleo ya nchi, hivyo amewahimiza kutumia kikamilifu fursa mbalimbali zinazojitokeza, ikiwemo mikopo ya 10% inayotolewa na Halmashauri, ili kuanzisha na kuimarisha shughuli za kiuchumi zitakazowaongezea kipato na kuwatoa kwenye utegemezi.
Kuhusu changamoto ya mazingira duni kwa baadhi ya wajasiriamali wadogo, Mhe. Nanauka amesema Serikali inatambua mchango wao katika uchumi wa Taifa, hivyo itaendelea kuboresha mazingira ya kufanyia biashara ili kuhakikisha wanapata sehemu bora, salama na rafiki kwa maendeleo ya biashara zao.
Katika hatua nyingine, Mhe. Waziri amewataka vijana wa Kyela kulinda na kuthamini amani ya nchi kwa kujiepusha na vitendo vinavyoweza kusababisha vurugu au kuharibu miundombinu ya umma. Amesema amani ni msingi muhimu wa maendeleo na kila kijana ana wajibu wa kuilinda.
Bomani Street
Sanduku la Posta: P. O box 320 Kyela
Simu ya Mezani: 025-2540035/7
Simu ya Mkononi: 0713655466
Barua pepe: ded@kyeladc.go.tz
Haki miliki @2017 Halmashauri ya wilaya ya Kyela. Haki zote zimehifadhiwa