Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Mhe. Josephine Manase, ameendelea na ziara yake ya kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wa Wilaya Kyela, ambapo leo tarehe 14.07.2025 amefika katika Kijiji cha Kilombero Kata ya Mababu.
Katika Ziara hiyo, Mhe. Manase ametilia mkazo umuhimu wa utunzaji wa mazingira, ambapo amewataka wananchi kuacha mara moja ukataji miti kiholela pamoja na shughuli za kilimo katika maeneo ya milima. Amesema kuwa tabia hizo zinaweza kusababisha mmomonyoko wa ardhi na maafa makubwa kama maporomoko ya ardhi au mafuriko.
Aidha, katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, DC Manase amewataka wananchi kuendelea kulinda amani. Ameonya dhidi ya kujiingiza kwenye siasa chafu ambazo zinaweza kuhatarisha utulivu na mshikamano tulionao, akisisitiza kuwa amani ni msingi wa maendeleo ya taifa lolote duniani. Vilevile, DC Manase amewaasa wananchi kuchagua viongozi wenye maono, watakaokuwa tayari kuleta maendeleo katika taifa letu na kuwa pamoja na wananchi katika shida na ra
Katika hatua nyingine, DC Manase amewahimiza wananchi kujiunga na Bima ya Afya ya Jamii (ICHF) kwa gharama ya shilingi elfu 30 kwa watu sita wa familia moja. Amesema kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kupunguza gharama za matibabu na kuhakikisha huduma bora za afya kwa kila mwananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, Adv. Florah A. Luhala, alieleza kuwa tayari Halmashauri imeshapeleka shilingi milioni 30 kwa ajili ya umaliziaji wa ujenzi wa madarasa ya Shule ya Msingi Kilombero, na ameahidi kukamilisha shilingi milioni 20 zilizobaki ili kuhakikisha shule hiyo inakamilika kwa wakati na kuwahudumia wanafunzi ipasavyo.
Pia akijibu kero ya uhaba wa nyumba za walimu, Adv. Luhala amesema kuwa Serikali kupitia halmashauri hiyo tayari imeanza ujenzi wa nyumba mbalimbali kwa walimu wa sekondari, ikiwemo Shule ya Sekondari Ibanda, Shule ya Sekondari Bondeni, na Shule ya Sekondari Mbeya Girls. Amesema kuwa mara tu bajeti ijayo Serikali itakapotoa fedha, halmashauri itashauri kuanza ujenzi wa nyumba za walimu wa shule za msingi ili kuboresha mazingira ya kufundishia kwa walimu katika ngazi zote.
Bomani Street
Sanduku la Posta: P. O box 320 Kyela
Simu ya Mezani: 025-2540035/7
Simu ya Mkononi: 0713655466
Barua pepe: ded@kyeladc.go.tz
Haki miliki @2017 Halmashauri ya wilaya ya Kyela. Haki zote zimehifadhiwa