Mkuu wa wilaya ya Kyela Mheshimiwa Ismail Mlawa, amekabidhi pikipiki 11 zilizonunuliwa kwa fedha za mikopo inayokana na 10% ya mapato ya ndani kwa vikundi 2 vya bodaboda hapa wilayani kyela, pikipiki hizo zimekabidhiwa siku ya jumatatu tarehe 13/12/2021 katika viwanja vya Halmashauri ya wilaya ya Kyela.
Akikabidhi pikipiki hizo Mheshimiwa Ismail Mlawa amesema;
Anamshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan, kwa uwezo wake mkubwa wa kusimamia Ilani ya Chama Tawala, Ilani inayozitaka Halmashauri zote kutenga 10% ya mapato ya ndani ili kutoa mikopo kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Na kwa kupitia mapato hayo leo hii halmashauri yetu imeweza kutoa pikipiki 11 kwa vikundi 2 vya vijana.
Amesema, “Mheshimiwa Rais aliposema kazi iendelee, alimaananisha kwani kuendelea kwenyewe ndio huku sasa”.
Pamoja na hayo aliwaasa wanavikundi hao kwenda kuzitumia pikipiki hizo katika kazi ambazo zitawasaidia kupata kipato chao kwa njia halali, kinyume na hapo sheria itachukua mkondo wake.
Aidha Mwenyekiti wa Halmashauri Mheshimiwa katule G. Kingamkono alitoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mkuu wa wilaya, Mheshimiwa Mbunge, Mkurungenzi mtendaji pamoja na Afisa maendeleo ya jamii wa wilaya kwa utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, hadi kufanikiwa kutoa mikopo yenye tija kama hii.
Pia aliwaasa wanufaika wa mkopo (bodaboda) kuwa waumini wa kulinda mapato ya serikali yasitoroshwe, kwani mikopo hii inapatikana kwa kupitia fedha za makusanyo ya mapato ya ndani. Pamoja na hayo Mheshimiwa Mwenyekiti, aliwahakikishia wananchi kwamba Halmashauri ya wilaya imejipanga katika kutoa mikopo yenye tija kwa kila robo ya mwaka, hivyo ni kazi ya vikundi kujipanga na kupata mikopo hiyo.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kyela Ndugu Ezekiel Magehema amesema, anaishukuru serikali kwa kutenga 10% ya mapato ya ndani kwa ajili ya kutoa mikopo kwa makundi maalum, na halmashauri yetu inayatekeleza hayo. Kwani kwa kipindi hiki halmashauri imetoa shilingi 150,000,000/=, pesa zilizotolewa kwa kufuata taratibu zote za vikao vya kisheria kwa ajili ya mikopo kwa makundi ya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu.
Mwisho ndugu Mbwana Limposo kiongozi wa moja kati ya wanavikundi hao, alitoa shukrani zake za dhati kwa viongozi na serikali na kusema, wanashukuru kwa kupata pikipiki hizi kwani kwa sasa wameepukana na pikpiki za malengo.
Bomani Street
Sanduku la Posta: P. O box 320 Kyela
Simu ya Mezani: 025-2540035/7
Simu ya Mkononi: 0713655466
Barua pepe: ded@kyeladc.go.tz
Haki miliki @2017 Halmashauri ya wilaya ya Kyela. Haki zote zimehifadhiwa