Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kyela, Mhe. Josephine Manase, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya, amepokea boti mpya ya doria iliyokabidhiwa na Jeshi la Polisi Tanzania leo, tarehe 23 Agosti 2025, katika Ziwa Nyasa, Kiwira Port.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Manase ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuongeza vifaa vya kuimarisha ulinzi na usalama katika Ziwa Nyasa.
Amesema boti hiyo itaongeza nguvu katika kuhakikisha usalama wa Ziwa Nyasa unasimamiwa ipasavyo, ikiwa ni pamoja na kudhibiti vitendo vya uhalifu vinavyofanywa na watu wachache wenye nia ovu. Aidha, amezitaka taasisi zote za ulinzi na usalama wilayani humo kuhakikisha boti hiyo inatunzwa na kutumika kwa ufanisi ili idumu kwa muda mrefu na kuleta manufaa kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamini Kuzaga, amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama wilayani Kyela, ikiwemo Jeshi la Uhamiaji na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kulitumia vyema boti hilo katika kuimarisha doria na kutokomeza uhalifu unaotokea kupitia Ziwa Nyasa, ikiwemo uvukaji haramu wa mipaka.
Ikumbukwe kuwa Ziwa Nyasa ni miongoni mwa maziwa makubwa nchini Tanzania, na kwa upande wa Wilaya ya Kyela linapakana na nchi ya Malawi. Uwepo wa boti hilo utarahisisha doria za mara kwa mara, kusaidia kudhibiti wahamiaji haramu na kulinda mipaka ya taifa kupitia ziwa hilo.
Bomani Street
Sanduku la Posta: P. O box 320 Kyela
Simu ya Mezani: 025-2540035/7
Simu ya Mkononi: 0713655466
Barua pepe: ded@kyeladc.go.tz
Haki miliki @2017 Halmashauri ya wilaya ya Kyela. Haki zote zimehifadhiwa