Mkuu wa wilaya ya Kyela, Josephine Manase,amesema hadi kufikia Mei 3, mwaka huu, wanafunzi 189 waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza wilayani humo, bado hawajaripoti shuleni.
Amesema lakini licha ya changamoto hiyo, wanatakiwa wajipongeze kwani wanafunzi wengi wameitikia wito wa kwenda kuripoti kidato cha kwanza.
Mhe.Josephine aliyasema hayo wakati akitoa salamu zake katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Kyela, kilichofanyika tarehe 04/05/2023 katika ukumbi wa halmashauri uliopo Kyela mjini.
Amesema wazazi ambao hawajawapeleka watoto wao kuripoti shule, tunaishi nao katika jamii, na wengi wao ukiangalia sababu wanazozitoa siyo za msingi, kwani Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewafanyia elimu bure sasa kwa nini wazazi wanakuwa wagumu, kutoa watoto kwenda kuhudhuria masomo darasani.
“Lakini pia sisi kama viongozi tujaribu kuongea na wazazi, na kuwaelimisha kwamba elimu ni muhimu kwa ajili ya watoto wetu, wanapopata elimu wao ndiyo wanaokuwa viongozi wetu wa baadaye, bila wao kupata elimu ina maana tunajenga taifa lisilokuwa na uwezo” alisema Manase.
Awali Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kyela Mheshimiwa Katule G. Kingamkono, amesema kutokana na Mradi wa ujenzi wa wodi ya Mama na mtoto kusuasua Baraza la Waheshimiwa Madiwani linatoa tamko kwamba mkurugenzi wa halmashauri Kyela, afanye maamuzi ya haraka kuvunja mkataba na TBA, Lakini kama TBA watarudi kazini kwa kasi waendelee, Ila kama wataendelea kusuasua wavunje mkataba mapema, sababu fedha ipo na kila kitu kipo ila kasoro yeye TBA, haleti mafundi kwa wakati .
Aliongeza ni aibu kwani Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, anahangaika kutafuta na kuwapelekea fedha lakini wao kama viongozi (madiwani), wanatakiwa kuweza kuzisimamia vizuri fedha hizo ili huduma ziweze kuwafikia wananchi.
“Utendaji kazi wa TBA siyo mzuri ndiyo maana tumetoa maelekezo, kama baraza na bahati nzuri niliutembelea mradi kama wiki moja iliyopita, na pia tulishawaambia TBA kama wataendelea kusuasua basi ni vizuri tuvunje mkataba, ili tuendelee kuweka taratibu nyingine” alisema Kingamkono.
Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri Kyela, Kenneth Nzilano, amesema Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea kuwasapoti kwa kutoa fedha nyingi, kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali zikiwemo shule, madarasa, zahanati lakini pia hospitali ya wilaya hiyo.
Nzilano alisema ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika hospitali ya wilaya, jengo lililoanza kujengwa mwaka 2020/2021, na jengo hilo kwa sasa lipo katika hatua za mwisho.
“Jengo halijaenda katika hatua ambazo zilikuwa zinahitajika, sababu ya ucheleweshwaji wa fundi mjenzi ambaye ni TBA, tumekaa naye kwamba kama hataweza kwenda na kasi tunayoitaka sisi, kama halmashauri ya kukamilisha jengo kwa wakati , basi tutafika mahali ambapo tutachukua hatua za kusimamisha mkataba wake” alisema Nzilano
Bomani Street
Sanduku la Posta: P. O box 320 Kyela
Simu ya Mezani: 025-2540035/7
Simu ya Mkononi: 0713655466
Barua pepe: ded@kyeladc.go.tz
Haki miliki @2017 Halmashauri ya wilaya ya Kyela. Haki zote zimehifadhiwa