MKUU wa wilaya Kyela, Mhe. Josephine Manase, amewataka madiwani, watumishi na wataalamu wa halmashauri ya wilaya ya Kyela , kuendelea kuchapa kazi kwa bidii na weledi, ili kuhakikisha wanakwenda kutimiza adhma ya Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ya kuwaletea maendeleo wananchi.
Amesema jambo hilo limekuwa linafanikiwa, kutokana na uwepo wa amani ndani ya wilaya, ambapo katika hilo madiwani nao wanao mchango mkubwa kuhakikisha wilaya inakuwa na utulivu.
Mhe. Josephine ameyasema hayo wakati akitoa salamu zake, katika baraza la madiwani lililofanyika tarehe 31/10/2023wa katika ukumbi wa mikutano uliopo Kyela mjini.
“Napenda kutoa shukrani nyingi kwa Rais Dk.Samia, kwa miradi mikubwa inayoendelea kutekelezwa wilayani hapa ikiwemo ile ya elimu, afya na barabara” alisema Josephine.
Aliongeza wote ni mashahidi kwani upande wa elimu, wanayo shule ambayo wanaendelea kuijenga katika kata ya Busale, ambayo hadi sasa tayari serikali imepeleka Tshs bilioni 3.
Mhe. Josephine amesema shule hiyo itakapokamilika ujenzi wake, itakwenda kubadirisha sura nzima eneo la kata ya Busale na kuwaomba madiwani wote kuitembelea na kujionea kazi kubwa ambayo Rais Dk.Samia anaifanya.
“Shule ile itakwenda kuwa ya wasichana kimkoa, na tutakwenda kupokea wanafunzi kutoka sehemu mbalimbali na mradi huo tunategemea utakamilika mwezi Desemba mwaka huu ili Januari tuweze kupokea wanafunzi” alisema Josehine.
Mheshimiwa Mkuu wa wilaya amesema, ujenzi wa shule ya sekondari katika kata ya Ibanda upo katika hatua za mwisho za upauaji na kumpongeza Mheshimiwa diwani wa kata ya Ibanda kwa namna ameendelea kutoa ushirikiano ili kuhakikisha mradi huo unakamilika.
Mhe. Josephine amesema mradi huo, umepelekea huduma mbalimbali kufika kata ya Ibanda, ikiwemo umeme ambao ukifika shuleni hapo basi utakwenda pia kusogezwa kwa wananchi.
“Tunawashukuru wananchi wa kata za Busale na Ibanda, kwa namna ambavyo wamekuwa wakijitoa, katika kushiriki kwao kuhakikisha miradi ile inakamilika kwa wakati” alisema Josephine.
Awali baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya Kyela mkoani Mbeya, lilimpongeza Mhe. Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, kuendelea kutatua changamoto za wananchi wilayani Kyela, kwa kutuletea miradi mbalimbali ya maji ili kumaliza kero ya maji.
Aidha Mwemyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kyela Mhe. Katule Kingamkono, amesema hivi karibuni halmashauri imepokea mradi wa maji, ambao utahudumia zaidi ya vijiji 25, na hivi sasa utekelezaji wake unaendelea kufanyika, licha ya awali mkandarasi anayeujenga kupatwa na changamoto wakati wa uchimbaji mitaro.
“Sasa hivi mradi upo katika hatua ya utandazaji wa mabomba, tutaendelea kuwasiliana na mamlaka husika waendelee kumuongezea nguvu mkandarasi ili utekelezaji wake ukae vizuri” alisema Kingamkono.
Mhe. Kingamkono alisema matumaini yao ni kwamba, mradi huo wa maji utakamilika wakati wowote kuanzia sasa sababu anaamini serikali ya Mhe. Rais Dk.Samia inatoa fedha.
Kuhusu kupandishwa hadhi kwa mamlaka ya mji mdogo wa Kyela, Kingamkono amesema hilo lipo katika uwezo wa mamlaka ya serikali kupitia ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na mamlaka nyingine.
Mwisho alitoa pongezi kwa watumishi wote pamoja na viongozi kwa ushirikiano na uchapakazi unaoleta maendeleo ya kweli wilayani Kyela.
Bomani Street
Sanduku la Posta: P. O box 320 Kyela
Simu ya Mezani: 025-2540035/7
Simu ya Mkononi: 0713655466
Barua pepe: ded@kyeladc.go.tz
Haki miliki @2017 Halmashauri ya wilaya ya Kyela. Haki zote zimehifadhiwa