(picha kutoka Maktaba)
Mkuu wa wilaya ya Kyela Mhe. Josephine Manase amewataka wataalam wa afya kuwahamasisha wananchi kuchukua tahadhari ili kujikinga na magonjwa yasiyo pewa kipaumbele, ikiwemo ugonjwa wa kichocho, magonjwa ya minyoo ya tumbo hasa kwa watoto chini ya umri wa miaka 15.
Mhe. Josephine Manase ameyazungumza hayo leo tarehe 26/02/2024 katika kikao cha "PHC" kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri, kikiwa na lengo la kupanga mpango mkakati wa zoezi la umezeshaji dawa za kichocho na minyoo ya tumbo shuleni. Ambapo wilaya ya Kyela inatarajia kuwafikia watoto 49769.
Aidha Mhe. Mkuu wa wilaya ya Kyela amewataka wataalam wa afya, kutoa Elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa uwepo wa choo kwa kila kaya, kwani kwa kufanya hivyo, kutapunguza kuenea kwa magonjwa.
Vilevile Mhe. Manase amewaomba wataalam hao kuwahamasisha wananchi kuwa na utaratibu ya kupima afya mara kwa mara ili kupunguza athari zitokanazo na magonjwa yasiopewa kipaumbele.
Pamoja na hayo Mhe. Manase amewasisitiza wananchi kuepuka imani potofu, kwani kuna baadhi ya jamii bado zina imani potofu ambazo hupelekea madhara makubwa katika jamii.
"Kuna jamii zinaamini kuwa mtoto akikojoa damu basi inaonekana mtoto amekua rijali yani amebaleghe ambapo jambo hilo si lakweli" Amesema Mhe. Manase.
Hata hivyo Mhe. Mkuu wa wilaya ametoa shukrani kwa Mhe. Rais na serikali ya awamu ya sita, kwa namna inavyojali wananchi hata kufanya haya mazoezi ya chanjo na umezaji dawa, ili kulinda jamii na watoto wetu dhidi ya magonjwa mbalimbali yasiyopewa kipaumbele.
Aidha amewaomba viongozi wa dini kutumia nafasi zao katika kuisaidia serikali kufikisha Elimu kwa waumini wao ili kupata jamii ambayo itafahamu kwa ukaribu magonjwa haya yasiyopewa kipaumbele na kuchukulia tahadhari.
Mwisho Mhe. Manase amesema kwa kuzingatia njia zote za kujikinga au kupiga vita magonjwa haya hususani magonjwa ya kichocho na minyoo ya tumbo wilaya ya Kyela, inaweza ikatokomeza magonjwa haya na kusiwe na maambukizi yoyote.
Kwani Serikali imetumia gharama kubwa kuhakikisha inatokomeza magonjwa haya ili wananchi wake waishi vizuri, na kutengeneza kizazi chenye afya nzuri ya mwili na akili.
Bomani Street
Sanduku la Posta: P. O box 320 Kyela
Simu ya Mezani: 025-2540035/7
Simu ya Mkononi: 0713655466
Barua pepe: ded@kyeladc.go.tz
Haki miliki @2017 Halmashauri ya wilaya ya Kyela. Haki zote zimehifadhiwa