Mkuu wa wilaya ya Kyela Mheshimiwa Ismail Mlawa, akiongea kwa uchungu juu ya wanafunzi wanaotoka kata ya Busale kwenda kusoma kijiji cha Ilima ambapo pana umbali mrefu
Mkuu wa wilaya ya Kyela Mheshimiwa Ismail Mlawa amezindua ujenzi wa madarasa 67 tarehe 08/11/2021, ujenzi utakaofanyika katika shule za sekondari 21 hapa wilayani Kyela. Akizungumza na wananchi waliojaa katika eneo la viwanja vya shule ya sekondari Busale, Mheshimiwa Mkuu wa wilaya amesema, Rais wa Jamuhuri Ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suruhu Hassan ametoa fedha itakayojenga madarasa 67 katika wilaya ya Kyela, hivyo sisi wanaKyela yatupasa kumuunga mkono Mheshimiwa Rais wetu kwa kujitolea kwa nguvu zote ili kuhakikisha ujenzi wa vyumba hivi vya madarasa unakamilika kwa wakati.
Aidha Mheshimiwa Mkuu wa wilaya ya Kyela hakusita kutoa pongezi kwa wananchi wa kata ya Busale, wakisimamiwa na diwani wao Mheshimiwa Adam Kabeta, ambae amekuwa mstari wa mbele katika kuanzisha miradi mingi ya maendeleo katika kata hiyo, na miradi yote ikiwa inatekelezwa kwa kasi kubwa. Hadi sasa kata ya Busale ina shule 2 za sekondari.
Mkuu wa wilaya ya Kyela Mheshimiwa Ismail Mlawa (kuhoto), Katibu Tawala (katikati), Mheshimiwa diwani Adam Kabeta kata ya Busale(kulia) na Mkurugenzi Mtendaji Ndugu Ezekiel Magehema (Nyuma) wakiwaongoza wananchi kuelekea eneo la ujenzi wa vyumba vya madarasa kufanya kazi.
Pamoja na hayo Mkuu wa wilaya ya Kyela aliwakumbusha wasimamizi wa pesa za ujenzi wa vyumba vya madarasa hayo, kuzitumia pesa hizo kadiri zilivyopangwa kutumika. Kinyume na matumizi hayo basi sheria itachukua mkondo wake. Akionesha kuguswa kwake na jinsi wananchi wa kata ya Busale wanavyojitokeza katika shughuli za maendeleo, Mkuu wa wilaya ya Kyela alitoa shilingi 50,000/= kuajili ya maji kwa mafundi waliokuwa wakiendelea na kazi ya ujenzi. Hata hivyo, Mheshimiwa Mkuu wa wilaya aliungana na wananchi hao katika shuguli za nguvu kazi.
Mkuu wa wilaya Mheshimiwa Ismail Mlawa akisaidiana kazi na wananchi wa kata ya Busale katika ujenzi wa vyumba vya madarasa
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kyela Ndugu Ezekieli Magehema alitoa pongezi zake za dhati kwa wananchi wa kata ya Busale kwa namna wanavyoshirikiana katika shughuli za maendeleo ya kata yao. Pia alimuhakikishia Mheshimiwa Mkuu wa wilaya kuwa atakuwa sambamba kwa kila eneo ambapo pesa hizi zinakopelekwa kwa ujenzi wa madarasa, ili kusaidia ujenzi kwenda kwa haraka na kwa tija.
Mkurugenzi Mtendaji ndugu Ezekiel Magehema akisaidiana kazi na wananchi wa kata ya Busale katika ujenzi wa vyumba vya madarasa
Mwisho mganga Mkuu wa hospitari ya wilaya Bi. Mariam Ngwere, alipata fulsa ya kutoa elimu juu ya umuhimu wa kuchanja chanjo ya UVIKO 19, ikiwa ni hiari kwa kila mwananchi kuchanja chanjo hiyo mara tu baada ya kupata elimu.
Mganga Mkuu wa Hospitari ya wilaya ya Kyela akitoa elimu juu ya chanjo ya UVIKO 19 katika uzinduzi wa ujenzi wa vyumba 67 vya madarasa katika kata ya Busale
Bomani Street
Sanduku la Posta: P. O box 320 Kyela
Simu ya Mezani: 025-2540035/7
Simu ya Mkononi: 0713655466
Barua pepe: ded@kyeladc.go.tz
Haki miliki @2017 Halmashauri ya wilaya ya Kyela. Haki zote zimehifadhiwa