Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Mhe. Josephine Manase, amekabidhi hundi ya mfano yenye thamani ya shilingi milioni mia sita hamsini na tatu laki sita (653,600,000/=) kwa vikundi 70 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Hafla hiyo imefanyika tarehe 22 Septemba 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela.
Akizungumza wakati wa makabidhiano, Mhe. Manase alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuleta mkopo wa 10% wenye tija kwa wananchi. Amesema mkopo huo ni chachu ya maendeleo kwani unawawezesha wananchi kujipatia mitaji ya kukuza kipato na kujikwamua kiuchumi.
Aidha, Mkuu wa Wilaya ameipongeza Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kyela kwa kusimamia ipasavyo fedha zinazotolewa kwa ajili ya mikopo hiyo. Vilevile, aliwataka wanufaika wote waliokidhi vigezo kuzingatia mafunzo waliyopatiwa na wataalamu ili kuepuka changamoto wakati wa urejeshaji wa mikopo.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Ndg. Keneth Nzilano aliwataka wanufaika kuwa mabalozi wazuri wa mikopo hiyo ya 10% inayotolewa na Halmashauri. Alisisitiza kuwa ni wajibu wa kila mnufaika kufanya shughuli zao kwa weledi na kuhakikisha marejesho yanakamilika kwa wakati ili na wengine wapate nafasi ya kunufaika.
Hatahivyo Wanufaika wa mikopo hiyo walito shukrani zao dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela. Walisema mkopo huo umethibitisha dhamira ya serikali ya kuwakumbuka wananchi wote bila kuacha makundi maalumu ambayo mara nyingi yamekuwa yakikosa fursa za kiuchumi.
Vilevile waliongeza kuwa mikopo hiyo itawawezesha kuanzisha miradi mipya, kuboresha biashara zao zilizopo na hatimaye kukuza vipato vyao. Waliahidi kutumia mkopo kwa nidhamu na kuhakikisha marejesho yanafanyika kwa wakati .
Bomani Street
Sanduku la Posta: P. O box 320 Kyela
Simu ya Mezani: 025-2540035/7
Simu ya Mkononi: 0713655466
Barua pepe: ded@kyeladc.go.tz
Haki miliki @2017 Halmashauri ya wilaya ya Kyela. Haki zote zimehifadhiwa