Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kyela Mheshimiwa Katule G. Kingamkono akizungumza na watendaji kata, watendaji wa vijiji na walezi wa kata(Wakuu wa Idara) hapa wilayani Kyela.
Walezi wa kata (wakuu wa Idara), Maafisa tarafa, watendaji wa kata pamoja na watendaji wa vijiji wakiwasikiliza viongozi katika kikao kazi.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kyela Mheshimiwa Katule G. Kingamkono, aongeza chachu ya ukusanyaji wa mapato kwa kutoa pongezi kwa Ofisi ya Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Ofisi ya Mheshimiwa Mbunge, Mkurugenzi Mtendaji ndugu Ezekiel Magehema, Mhazina wa wilaya ndugu Patrick Msafi, watendaji wa kata, walezi wa kata (wakuu wa idara na vitengo) pamoja na watendaji wa vijiji kwa ukusanyaji mzuri wa mapato katika mwaka wa fedha 2020/2021.
Pongezi hizo zimetolewa tarehe 04/11/2021 katika kikao kazi kilichoandaliwa maalum kwa kupongezana baina ya viongozi wote waliofanikisha kufikisha 104% ya makusanyo katika mwaka wa fedha 2020/2021.
Halmashauri ya wilaya ya Kyela kwa mwaka 2020/2021, ilitakiwa kukusanya shilingi 3,621,067.00/= kutokana na vyanzo vya ndani. Lakini ilifanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi 3,771,874,644/= ikiwa ni sawa na 104% ziada ya 4% sawa na shilingi 373,563,577.00/=, ambapo vyanzo lindwa ikiwa ni shilingi 1,325,230,035/= na vyanzo vingine shilingi 2,446,644,609/=.
Akiongea katika kikao kazi hicho Mheshimiwa mwenyekiti amesema, "Natambua kazi nzito iliyofanywa na viongozi wote hapa wilayani, kwa umoja wao tumefanikisha kufikisha asilimia 104 ya mapato ya halmashauri yetu, pamoja na mafanikio haya, nawaomba viongozi wote hasa watendaji wa kata na vijiji kuongeza nguvu ya ukusanyaji wa mapato katika mwaka 2021/2022, ili tupande zaidi ya mwaka 2020/2021". Alisema, hii ni pamoja na kuzingatia suala la kupeleka mapato hayo Benk mara tu baada ya kuyakusanya.
Pia aliwaomba watendaji kata na vijiji kumuhakikishia katika kufanya kazi ya ukusanyaji wa mapato katika mwaka huu wa fedha. Ambapo watendaji hao walimuahidi kufanya vizuri zaidi ya mwaka wa 2020/2021.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kyela Ndugu Ezekiel H. Magehema, alitoa shukrani zake za dhati kwa viongozi wote wa wilaya ya Kyela kwa ushirikiano waliouonyesha hadi kufia 104% ya mapato katika mwaka wa fedha 2020/2021. Aidha alitoa pongezi nyingi kwa watendaji wa kata pamoja na kikosi kazi cha mapato kwani walifanya kazi kwa ushirikiano mkubwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kyela Ndugu Ezekiel H. Magehema, akiongea na watendaji kata, watendaji wa vijiji na walezi wa kata(Wakuu wa Idara) hapa wilayani Kyela.
Pamoja na hayo Mkurugenzi Mtendaji aliwataka watendaji wa kata na vijiji wasiokuwa na POS kufika ofisini na kuchukua POS kwani kwa sasa halmashauri yetu ina POS za kutosha.
Sambamba na hayo pongezi zilitolewa kwa kata ya Njisi, Ikimba, Ipinda na Kajunjumele kata zilizoongoza kwa ukusanyaji wa mapato. Na kwa kuonyesha furaha kubwa na imani kubwa kwa watendaji, Mkurugenzi Mtendaji alitoa ofa kwa watendaji na walezi wa kata kuandaa mchezo wa mpira wa miguu.
Mchezo utakaowakutanisha viongozi kwa umoja wao, ili kuongeza nguvu ya ushirikiano baina yao, Pia alisema atatoa ng'ombe wa kuchinja ili kufurahi na kubadilishana mawazo kwa pamoja.
Mwisho Mwenyekiti wa watendaji ndugu Temba aliupongeza uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Kyela kwa kutambua jitihada zinazofanywa na watendaji katika suala la ukusanyaji wa mapato na kuahidi kuongeza nguvu zaidi ili kuvunja rekodi ya ukusanyaji wa mapato wa mwaka wa fedha 2020/2021.
Bomani Street
Sanduku la Posta: P. O box 320 Kyela
Simu ya Mezani: 025-2540035/7
Simu ya Mkononi: 0713655466
Barua pepe: ded@kyeladc.go.tz
Haki miliki @2017 Halmashauri ya wilaya ya Kyela. Haki zote zimehifadhiwa