Mkuu wa wilaya ya Kyela, Mheshimiwa Josephine Keenja Manase amefanya ukaguzi katika mradi wa ujenzi wa kituo cha afya cha Njisi kilichopo kata ya Njisi hapa wilayani tarehe 23/02/2023.
Katika ukaguzi wake Mheshimiwa manase ametoa pongezi kwa kamati ya Ujenzi kwa hatua nzuri walipofikia katika ujenzi wa mradi huo.
Aidha Mheshimiwa mkuu wa wilaya amesema, lengo la kutembelea mradi huo ni kutaka kujihakikishia kama shughuli za ujenzi zinaendelea kama zilivyopangwa, Na kuitaka kamati hiyo kuto muangusha katika umaliziaji wa ujenzi wa mradi huo.
Hata hivyo Mheshimiwa Mkuu wa wilaya ya Kyela, ametoa shukrani zake za dhati kwa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa shilingi milioni 500 katika mradi huo, Na imani yake ni kwamba, mradi ukiisha kwa wakati na kwa kiwango cha juu, Mhe. Rais anapata imani ya kutupa hela za kuanzisha miradi mingine katika wilaya yetu.
Pamoja na hayo Mheshimiwa Manase amewataka kukamilisha kwa wakati eneo la chumba cha mionzi (X-ray) kwa kutengeneza njia (walk way) ili kiweze kuanza kutoa huduma, kwani mitambo imeshafungwa katika chumba hicho.
Aidha Mheshimiwa ametoa shukrani kwa Mkuu wa mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Zuberi Homera kwa kuujali mradi huo na kuwapenda wananchi wa kata ya Njisi kwa kujitolea nguvu zao katika ujenzi wa mradi huo.
Mwisho Mheshimiwa Mkuu wa wilaya ameridhishwa na kasi kubwa ya umaliziaji wa jengo la mama na mtoto na kuwahimiza kamati ya ujenzi kuendelea na kasi ya usimamizi wa kazi hiyo ili kuukamilisha mradi kwa wakati.
Nae diwani wa kata hiyo Mheshimiwa Omary Mwijuma, amemuomba mkuu wa wilaya Mheshimiwa Manase, kuwakumbuka katika kuanza ujenzi wa nyumba za watumishi katika kituo hicho cha afya mara baada ya kukamilika kwa awamu ya ujenzi inayoendelea.
Bomani Street
Sanduku la Posta: P. O box 320 Kyela
Simu ya Mezani: 025-2540035/7
Simu ya Mkononi: 0713655466
Barua pepe: ded@kyeladc.go.tz
Haki miliki @2017 Halmashauri ya wilaya ya Kyela. Haki zote zimehifadhiwa