HALMASHAURI ya wilaya Kyela, imezalisha miche bora 33,708 ya zao la Mchikichi, ambayo itagawiwa bure kwa wananchi ili kuwainua kiuchumi, ambayo itapandwa katika ekari 674.4, sawa na miche 50 kwa kila ekari moja.
Imeelezwa lengo la kufanya hivyo ni kuongeza uzalishaji wa zao hilo, ambalo limekuwa ni chanzo kikubwa cha mapato yake ya ndani.
Akizungumza wakati akizindua rasmi ugawaji wa miche hiyo kwa wananchi, mkuu wa wilaya Kyela, Josephine Keenja Manase, amesema mbegu ya zamani ilikuwa inachukua muda mrefu kukua, lakini baada ya kukaa na watalaam wa utafiti kutoka TARI, wameweza kupata mbegu bora.
Josephine amesema mbegu hiyo ni bora, na ukuaji wake unachukua muda mfupi na kuipongeza halmashauri kwa kuamua kuigawa miche hiyo kwa wananchi ili zao hilo, likikua liweze kusaidia kuinua kipato cha mwananchi mmoja mmoja.
Aliongeza kwamba taifa kwa jumla litanufaika, kwani michikichi hiyo ni zao la kiuchumi, hivyo litasaidia kupunguza gharama ya serikali kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi, na badala yake yatakuwa yanakamuliwa humu humu nchini, hususani wilayani Kyela.
“Nitilie mkazo kwamba wananchi wote, pamoja na kwamba tunachukua hii miche ya miti ya michikichi, basi tuhakikishe tunaitunza, lengo ni kuhakikisha tunakwenda kufikia lengo la kupata tani zinazohitajika za mafuta ya kula kwa mwaka” alisema Josephine.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya Kyela, Katule Kingamkono, amesema lengo lao ni mambo mawili, la kwanza ni kuchochea uchumi wa mwananchi mmoja mmoja, lakini pili kuongeza mapato ya halmashauri na ili waweze kwenda mbele ni lazima waanze maandalizi ya uwekezaji.
Kingamkono alibainisha hivi sasa wanayo miche bora ya michikichi, ambayo wataalamu wamejitahidi kuiboresha zaidi, na ndoto yao ni kuwa kufikia mwaka 2025 wanavyohitimisha baraza la madiwani, wawe na michikichi zaidi ya 500,000 ama milioni moja.
“Tunaamini michikichi hiyo baada ya miaka mingine ijayo, halmashauri ya wilaya Kyela kimapato haitakuwa hapa ilipo sasa hivi” alisema Kingamkono.
Ofisa Kilimo wa wilaya Kyela, Kenneth Nzilamo, alisema katika msimu wa kilimo wa mwaka 2021/2022,halmashauri ilizalisha miche ya michikichi 35,552 ambayo iligawiwa bure kwa wananchi 941, kwa kushirikiana na taasisi ya utafiti TARI Uyole na TARI Kihinga.
Alisema zao hilo kwa halmashauri ya wilaya Kyela, ni chanzo kikubwa cha mapato na kutoa mfano mwaka 2019/2020 zaidi ya sh.milioni 80.9 zilizalishwa, na mwaka 2020/2021 zaidi ya sh.milioni 183.2 zilizalishwa.
“Kwa mwaka 2021/2022 zaidi ya sh.milioni 135.9, ilizalishwa na katika msimu 2022/2023 tunatarajia kukusanya jumla ya sh.milioni 127.2, na eneo linalolimwa michikichi ni jumla ya hekta 1, 500, ambapo uzalishaji wake kwa wastani ni tani 2,125” alisema Nzilano.
Mkulima wa zao hilo mkazi wa kata ya Ngana, Aden Kajela ambae ni diwani wakata hiyo, alisema anamshukuru Rais Dk.Samia kwa mpango huo mzuri wa kuwaboreshea wakulima, namna ya upatikanaji wa uchumi bora.
Kajela aliongeza kupitia miche hiyo ya michikichi, wanatarajia kwamba itawazalishia mafuta ya kula na mbali ya hilo, watatengeneza mbosa na kupata mafuta ya kutengenezea sabuni, na kuwa miti hiyo ya michikichi ina faida kubwa sana.
“Sababu tulikuwa na mbegu ya michikichi ya zamani, na sasa tumepata ya kisasa ambayo itatuondoa katika hali ya umaskini na kutuleta katika hali bora ya kiuchumi ambayo itatufanya tuwe na uchumi endelevu” alisema Kajela.
Mwisho.
Bomani Street
Sanduku la Posta: P. O box 320 Kyela
Simu ya Mezani: 025-2540035/7
Simu ya Mkononi: 0713655466
Barua pepe: ded@kyeladc.go.tz
Haki miliki @2017 Halmashauri ya wilaya ya Kyela. Haki zote zimehifadhiwa