Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jami Jinsia, Wazee na Watoto (MB), Mheshimiwa Mwanaid Ali Khamis, amefanya ziara tarehe 08/10/2021 hapa wilayani Kyela, na kutembelea mradi wa ujenzi wa kituo cha afya unaotekelezwa katika kata ya Itunge.
Akizungumza na wananchi wa kata ya Itunge, Mheshimiwa Naibu waziri (MB), amewaomba wananchi wa kata ya Itunge kuendelea kushirikiana na kudumisha umoja walionao, ili kukamilisha ujenzi wa kituo cha cha afya, ambacho wameanza kukijenga kwa kasi kubwa, na ujenzi huo uweze kukamilika kwa wakati.
Amesema; “Ujenzi wa kituo hiki cha afya si mali ya wanaitunge wanaokijenga sasa, bali kituo hiki ni urithi kwa jamii nzima na kizazi kijacho” pamoja na hayo Mheshimiwa Naibu Waziri (MB), amesema serikali inawapenda wananchi wake hivyo, atahakikisha kituo cha afya itunge kinakamilika kwa wakati na alichangia ujenzi huo kwa kutoa mifuko 15 ya saruji. Pia aliwaagiza viongozi kutoka ngazi ya halmashauri kusimamia ujenzi huo ili kuhakikisha fedha iliyotolewa na serikali inatumika kama ilivyopangwa.
Aidha Mheshimiwa Mwanaid Ali Khamis amewakumbusha na kuwahamasisha wananchi wa kata ya Itunge kuzidi kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa UVIKO 19, kwa kuchanja kwani ugonjwa huu ni hatari sana kwa afya zetu, Pia aliwahakikishia wananchi wa Itunge kuwa, punde ujenzi wa kituo hicho utakapokamilika serikali italeta vifaa kwa ajili ya kutoa huduma za afya kituoni hapo.
Pamoja na hayo, Mheshimiwa Naibu Waziri aliwasisitiza wananchi kujitokeza na kutoa ushirikiano wa dhati katika zoezi la sensa ya watu na makazi itakayofanyika mwakani, ili kuhakikisha kila mwananchi anahesabiwa.
Nae Mkuu wa wilaya ya Kyela Mheshimiwa Ismail T. Mlawa aliahidi kuchangia shilingi 500,000/= kwa ujenzi wa kituo hicho cha afya, na kumuahidi mheshimiwa Naibu Waziri kusimamia ujenzi wa kituo hicho hadi kitakapokamilika. Pia alitoa shukrani zake za dhati kwa serikali ya Jamuhuri Ya Muungano Wa Tanzania kwa kuzidi kuikumbuka wilaya ya Kyela kwa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Aidha Mbunge wa jimbo la Kyela Mheshimiwa Ally M. Jumbe aliishukuru serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Wa Jamuhuri Ya Muungano Wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kusikiliza kilio chake dhidi ya uchache wa vituo vya afya Kyela, na sasa serikali inajenga vituo 2 vya afya Kyela. Pia alimshukuru Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kyela Mhe. Katule G. Kingamkono na Mkurugenzi Mtendaji ndugu Ezekieli H. Magehema, kwa kubali kupeleka fedha kwa ujenzi wa kituo cha afya katika kata ya Ngonga na kata ya Itunge.
Mwisho Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mheshimiwa Mwanaidi Ali Khamis (MB), aliweza kutembelea kikundi cha SHFA,kikundi kinachojishughulisha na utoaji wa elimu ya makuzi na malezi kwa watoto katika kata ya Mwanganyanga. Kikundi cha kilimo bidii cha wanawake katika kata ya Makwale, ili kujionea na kujifunza jinsi wanavyofanya kazi zao.
kikundi cha wanawake "Kilimo Bidii" wakimkabidhi Mheshimiwa Mwanaidi Ali Khamis Naibu Waziri(MB) mafuta ya mawese kama ishara ya konyesha sehemu yao ya utendaji wa kazi
Kikundi cha "SHFA" kikitoa burudani murua mbele ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Bomani Street
Sanduku la Posta: P. O box 320 Kyela
Simu ya Mezani: 025-2540035/7
Simu ya Mkononi: 0713655466
Barua pepe: ded@kyeladc.go.tz
Haki miliki @2017 Halmashauri ya wilaya ya Kyela. Haki zote zimehifadhiwa