WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema ujenzi wa barabara ya Ibanda-Kajunjumele,Kajunjumele-bandari ya Kiwira na Kajunjumele-bandari ya Itungi, wilayani Kyela, zenye urefu wa kilometa 32 kwa jumla, unatarajia kugharimu sh.bilioni 38.
Amesema barabara hizo zinazojengwa kwa kiwango cha lami, ni sehemu ya mtandao wa barabara muhimu za nchi inayounganisha mkoa wa Mbeya na mikoa ya Ruvuma na Njombe, kupitia Ziwa Nyasa katika bandari ya Itungi, Kiwira na Mbamba Bay.
Profesa Mbarawa aliyasema hayo jana tarehe 27/12/2022, mara baada ya kuushuhudia utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa barabara hizo, kati ya Mkurugenzi Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Rogatus Mativila na Meneja wa kampuni ya AVM-Dillingham International Inc., Mhandisi Umit Necat Pal. Mkataba uliosainiwa hadharani huku wananchi waliohudhuria katika hfla hiyo wakishuhudia. Na kwa mara ya kwanza Kyela imeandika historia ya uanzishwaji wa kusainisha mikataba ya serikali mbele ya wananchi.
Alisema barabara hiyo itakapokamilika itachochea shughuli za kiuchumi, kama vile usafirishaji wa bidhaa mbalimbali ikiwemo Kokoa, makaa ya mawe, mazao mbalimbali ya chakula na biashara, mazao ya misitu, uvuvi na shughuli za kijamii kwa ujumla.
“Leo tumeshuhudia muda mfupi uliopita, utiaji saini wa mkataba wa kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami, barabara ya Ibanda-Kajunjumele yenye urefu wa kilometa 22, Kajunjumele-Kiwira Port yenye urefu wa kilometa 6 na Kajunjumele-Itungi yenye urefu wa kilometa 4” alisema Profesa Mbarawa.
Aliongeza barabara zote jumla zina urefu wa kilometa 32, na ujenzi wake utafanyika kwa kutumia fedha za ndani kwa asilimia 100.
Alisema ujenzi utakapokamilika, utarahisisha shughuli mbalimbali za kiuchumi na za kijamii, kwa wananchi waioshio maeneo ya wilaya ya Kyela, Rungwe, Ruvuma na Njombe na inatarajiwa kuwa shughuli za kiuchumi za wananchi wanaoishi kandokando ya Ziwa Nyasa zitaimarika zaidi.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (sekta ya ujenzi), Mhandisi Godfrey Kasekenya, alisema Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, sasa ameamua kuifungua Tanzania, na ameamua kuifungua wilaya ya Kyela, mkoa wa Mbeya na mikoa yote ya nyanda za Juu Kusini.
“Rais Dk.Samia anataka ikiwezekana mtu akishusha mizigo yake bandari ya Mtwara, aje Tunduru, aje Songea, Mbinga, Mbamba Bay, lakini avuke na meli aje bandari za Kiwira ama ile ya Itungi wilayani Kyela, ataweza akaamua kwenda Kasumulu, anaweza akaamua kwenda wilayani Ileje, kwa maana ya Isongele kwenda nchini Malawi” alisema.
Aliongeza ama anaweza kwenda Tunduma-Sumbawanga hadi Kigoma, na hadi sasa kipande kitakachokuwa kimebaki cha vumbi ni kutoka Kasumulu hadi Isongele wilyani Ileje, kwa barabara yote lakini kwa kuanzia Tunduma kwenda maeneo mengine, wakandarasi wapo kazini.
Mkuu wa mkoa Mbeya, Juma Homera, alisema kwa utashi wake Rais Dk.Samia, anahakikisha kwamba mkoa huo unaletewa miradi kama kawaida na hususani katika wilaya hiyo ya Kyela, kwa lengo la kuufungua mpaka wa Kasumulu unaozitenganisha nchi za Tanzania, Malawi pamoja na mikoa mingine miwili (Njombe na Ruvuma).
“Tunamshukuru sana Rais Dk.Samia, ambaye amepanga kujenga barabara hii, na leo hii tunashuhudia utiaji saini wa mkataba kwa mara ya kwanza, unafanyika hadharani …” alisema Homera.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Rogatus Mativila, alisema barabara hiyo yenye jumla ya urefu wa kilometa 32, itajengwa kwa kiwango cha lami na mradi wa ujenzi wa barabara hizo ni moja ya mikakati ya serikali kuharakisha maendeleo ya nchi.
Bomani Street
Sanduku la Posta: P. O box 320 Kyela
Simu ya Mezani: 025-2540035/7
Simu ya Mkononi: 0713655466
Barua pepe: ded@kyeladc.go.tz
Haki miliki @2017 Halmashauri ya wilaya ya Kyela. Haki zote zimehifadhiwa