Shirika lisilokuwa la kiserikali la Tanzania Interfaith Partnership (TIP) limefanya mafunzo ya kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa Kipindupindu leo tarehe 20/03/2023, mafunzo yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya wilaya ya Kyela.
Mafunzo hayo yameshirikisha viongozi wa dini, walimu wanaofanya kazi katika shule za msingi na sekondari ambazo zipo katika maeneo ya mpakani baina ya Tanzania na Malawi. Ikiwa na lengo kubwa la kuwajengea uwezo wawezeshwaji hao ili waweze kwenda kutoa elimu katika maeneo wanayotoka hususani katika maeneo ya Makanisa, misikiti na shule zilizopo maeneo ya mpakani.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Mkuu wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Wilaya Dr. Saumu Kumbisaga amesema;
Anawashukuru wadau wa Tanzania Interfaith Partnership (TIP) kwa kuja kutoa elimu ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa kipindupindu, ugonjwa unaosumbua nchi ya jirani kwa sasa, kwani hii itakuwa ni mwanzo wa kutoa elimu kwa makundi makubwa kwa kupitia misikiti, shule pamoja na makanisa.
Hata hivyo amesema, anaamini timu yote inayopewa mafunzo leo, itakuwa ni timu yake ambayo atatembea nayo katika kutoa elimu ya kujikinga na ugonjwa huu wa kipindupindu ikiwa ni pamoja na magonjwa ya mlipuko kama korona.
"Ni vizuri sisi ambao tunapata elimu hii kuendelea kutoa elimu kwa wenzetu, elimu ya kuto fanya mikutano inayoshirikisha watu wengi na isiyokuwa ya lazima, kwani magonjwa ni mengi ikiwemo hata ugonjwa wa korona." Amesema Dr. Kumbisaga.
Aidha Dr. Kumbisaga amesema lengo la kushirikisha makundi haya, ni kuifanya Kyela iweze kufikiwa na elimu hii kwa haraka, na kuifanya Kyela salama na Tanzania kwa ujumla wake.
"Timu hii baada ya mafunzo tunawaomba mhakikishe mnakua mabalozi wa kusisitiza wazazi kupeleka watoto kupata chanjo mbalimbali kwani magonjwa mengine ya milipuko kama, polio, surua yanazuilika kwa chanjo". Amesema Dr. Saumu Kumbisaga.
Mwisho aliwatakia mafunzo mema washiriki wote wa mafunzo hayo.
Shirika la Tanzania Interfaith Partnership(TIP) ni Shirika lisilokuwa la Kiserikali linaloundwa na Taasisi Kuu nne za kidini Tanzania yaani, Jumuia Ya Kikristo Tanzania (CCT), Baraza La Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), BARAZA la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Na ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar ( MoZ), lengo la shirika au taasisi hii ni kutoa huduma kwa jamii, katika masuala ya Afya, Ustawi wa jamii na ulinzi wa watoto, kupitia miundo ya Taasisi za kidini.
Mwisho.
Bomani Street
Sanduku la Posta: P. O box 320 Kyela
Simu ya Mezani: 025-2540035/7
Simu ya Mkononi: 0713655466
Barua pepe: ded@kyeladc.go.tz
Haki miliki @2017 Halmashauri ya wilaya ya Kyela. Haki zote zimehifadhiwa