Katika kufanya maadhimisho ya wiki ya kuongeza uelewa kwa jamii juu ya kupambana na usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya matumizi yasiyo sahihi ya dawa, maadhimisho yanayoendelea kufanyika kuanzia tarehe 18/11/2023 hadi tarehe 24/11/2023, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Afya TMDA kwa kushirikiana na wadau wengine wametoa elimu ya usugu wa vimelea dhidi ya matumizi ya dawa katika maeneo mbalimbali hapa wilayani Kyela.
Akitoa elimu kwa wafanyabishara katika kata ya Mababu kijiji cha Ngyeke, Jofrey Kikoti mkaguzi wa dawa TMDA nyanda za juu kusini amesema,
Usugu wa vimelea ni hali ya vimelea vya magonjwa kustahamili nguvu ya dawa iliyokusudiwa kuuwa vimelea, hasa vimelea vinavyosababisha magonjwa kwa binadamu, mifugo, samaki, mimea pamoja na bacteria, fangasi, virusi na protozoa.
Aidha bwana Kikoti ameeleza kwamba, mambo yanayosababisha usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa, ni pamoja na mgonjwa kupewa au kutumia kiasi kidogo au kikubwa cha dawa zaidi ya ilivyokusudiwa.
Pia mgonjwa kutomaliza dozi ya dawa kama ilivyoelekezwa wakati wa matibabu, tabia ya mgonjwa au mfugaji kununua au kutumia dawa bila kupata ushauri wa wataalamu, matumizi ya dawa hususani antibaotiki kwenye chakula cha mifugo yasiyozingatia ushauri wa kitaalam kwa ajili ya kunenepesha au kuharakisha ukuaji wa mfugo.
Vile vile amesema, matumizi holela ya dawa mfano, kwenye kilimo cha bustani, kutupa dawa au mabaki ya dawa na vifungashio bila kufuata utaratibu.
Pamoja na hayo ndugu Kikoti ametoa njia mbalimbali za kukabiliana na matumizi holela ya dawa ikiwemo, kuepuka tabia ya kutibu mifugo mwenyewe bila kuzingatia ushauri wa wataalamu wa mifugo, ameshauri njia bora za ufugaji hasa unaozingatia chakula na matumizi bora ya chanjo.
Aidha ndugu Kikoti, amewafundisha wananchi kupunguza matumizi ya dawa yoyote kwa ajili ya kukinga magonjwa au kunenepesha mifugo bila ushauri kutoka kwa mtaalamu wa dawa.
Mwisho amewataka wananchi kuepuka matumizi holela ya dawa ili kuokoa maisha. Elimu hiyo itaendelea kutolewa katika maeneo mengine hadi siku ya kilele cha maadhimisho tarehe 24/11/2023.
Bomani Street
Sanduku la Posta: P. O box 320 Kyela
Simu ya Mezani: 025-2540035/7
Simu ya Mkononi: 0713655466
Barua pepe: ded@kyeladc.go.tz
Haki miliki @2017 Halmashauri ya wilaya ya Kyela. Haki zote zimehifadhiwa