Wakati watanzania wakiungana na washiriki wengine duniani kusherehekea sikukuu za Krismasi na Mwaka mpya,
Umoja wa Wanakyela waishio sehemu mbalimbali maarufu IBHASA, wametoa msaada wa mafuta na miwani kwa watu wenye Ualibino na kuungana nao katika kukabidhi vifaa tiba katika kituo cha afya Njisi, Pia kutoa msaada wa vitabu katika shule mpya ya msingi Kilambo iliyopo kata ya Njisi.
Haya yamefanyika tarehe 27/12/2023 katika kata ya Njisi, wakati umoja huo ukiwa hapa wilayani Kyela, kuendelea na shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwemo kuwafariji watu wenye shida.
Akizungumza kwa niaba ya mwenyekiti wa IBHASA Ndugu Vanesa Ngesienge, amesema, umekuwa ni utamaduni wao kila ifikapo mwisho wa mwaka, kukaa na watu wenye uhitaji mbalimbali ili kujua shida zao na kutatua baadhi ya shida ikiwemo, masuala ya elimu na afya.
Aidha ameongeza kwa kusema kuwa, vifaa hivyo vilivyotolewa vinathamani ya shilingi milioni 4.9, fedha zilizotokana na michango yao pia michango kutoka kwa wenzao waishio nje na ndani ya nchi.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa kituo cha afya Njisi Dr. Jonson Mganyizi, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kyela Bi.Florah Luhala , amewashukuru Wana IBHASA, kwa misaada yote waliyoitoa kwa kituo hicho cha Afya pamoja na shule.
Naye Mhe. diwani wa kata ya Njisi Omary Mwinjuma, ameungana na mganga mfawidhi kutoa shukrani kwa wanaIBHASA, kwa msaada walioutoa kwa wananchi wake, na kusema jambo lililofanyika ni ishara ya wazi ya kuunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya sita, chini ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kipenzi cha Watanzania.
Vilevile mwenyekiti wa "TASI" chama cha watu wenye Ualibino wilayani Kyela, ndugu, Bwigane Mwamasangula, amekipongeza kikundi cha IBHASA na kuwaomba kuendelea kuwakumbuka, kwani bado wanamahitaji mengi muhimu.
Bomani Street
Sanduku la Posta: P. O box 320 Kyela
Simu ya Mezani: 025-2540035/7
Simu ya Mkononi: 0713655466
Barua pepe: ded@kyeladc.go.tz
Haki miliki @2017 Halmashauri ya wilaya ya Kyela. Haki zote zimehifadhiwa