Mheshimiwa Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kyela Katule G. Kingamkono(kushoto) akizungumza machache na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kyela Bi. Florah A. Luhala (katikati) walipokuwa wakikagua miradi ya maendeleo.
Waheshimiwa Madiwani wilaya ya Kyela wametembelea na kukagua miradi ya maendeleo, ikiwa ni utekelezaji wa ziara za kutembelea na kukagua miradi kwa kipindi cha robo ya nne kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Ziara hiyo imefanyika tarehe 27 hadi 28/07/2023, ikijumuisha Kamati ya Elimu na Afya, Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira, Mkurugenzi Mtendaji Bi. Florah A. Luhala akiwa na wataalamu kutoka Idara mbalimbali za Halmashauri.
Waheshimiwa Madiwani na wataalamu wametembelea Mradi wa ukarabati wa kituo cha walimu (TRC) katika shule ya msingi Ikolo, mradi wenye thamani ya shilingi 22,000,000, Ujenzi wa vyumba 2 vya madarasa katika shule ya msingi Ipyana mradi wenye thamani ya shilingi 40,000,000, Ujenzi wa shule Mpya kata ya Njisi yenye thamani ya shilingi 538,500,000, Ukaguzi wa vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi 112,500,000 katika zahanati ya Kilasilo.
Baadhi ya vifaa tiba vilivyonunuliwa na kukaguliwa katika zahanati ya kilasilo kata ya Ikimba.
Pamoja na miradi hiyo, Miradi mingine iliyotembelewa na kaguliwa ni mradi wa taa za barabarani kata ya Bondeni njia panda Kapwili, Ukaguzi wa vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi 112,500,000, Kikundi cha vijana waliokopeshwa fedha kupitia mfuko wa kusaidia wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, na kununua bodaboda katika kata ya Ibanda, pamoja na ujenzi wa shule mpya ya msingi katika kata ya Ikimba.
Moja ya jengo la madarasa katika shule mpya ya msingi inayojengwa katika kata ya Ikimba.
Miradi yote iliyotembelewa na kukaguliwa imeridhiwa na waheshimiwa madiwani ikiwa ni pamoja na kutoa pongezi zao za dhati kwa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuleta fedha nyingi zinazotekeleza miradi mbalimbali katika wilaya ya Kyela.
Aidha waheshimiwa madiwani wametoa maagizo ikiwemo agizo la umaliziaji wa miradi ya maendeleo kwa ubora na kuzingatia muda uliyopangwa.
Mradi wa taa za barabarani katika eneo la njia panda Kapwili kata ya Bondeni.
Hayo yote yamepokelewa na timu nzima ya wataalamu wa halmashauri wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Bi. Florah A. Luhala, na kuwaahidi waheshimiwa kuyatekeleza kwa wakati maagizo na ushauri uliotolewa katika ziara hiyo.
Ziara hiyo itakamilishwa tarehe 31/07/2023 mara baada ya kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango kutembelea miradi.
Waheshimiwa Madiwani wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumaliza ziara ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo.
Bomani Street
Sanduku la Posta: P. O box 320 Kyela
Simu ya Mezani: 025-2540035/7
Simu ya Mkononi: 0713655466
Barua pepe: ded@kyeladc.go.tz
Haki miliki @2017 Halmashauri ya wilaya ya Kyela. Haki zote zimehifadhiwa