Wananchi wa kijiji cha Lubaga kilichopo katika kata ya Bujonde wilayani Kyela Mkoani Mbeya, wataendelea kunufaika na huduma ya maji baada ya kukamilika kwa ukarabati wa mradi wao wa maji ulioharibiwa wakati wa utengenezaji wa miundo mbinu ya barabara kijijini hapo.
Akizungumza kabla ya kukabidhi cheti kwa jumuia ya watumia maji ya Kijiji cha Lubaga (JUWAMALU) jana tarehe 29 /09/2020, Mratibu wa Mradi huo ndugu Atunosyege Adamson Mwakang'ata amesema;
Mradi wa maji wa Lubaga ulianza kutengenezwa mwaka 2011 na kukamilika mwaka 2013 na kuanza kutumika mwaka huo huo 2013 mwishoni, baada ya hapo mradi huu ulipata changamoto kidogo baada ya kuharibiwa kwa miundo mbinu yake, wakati wa ukarabati wa barabara katika kijiji cha Lubaga na kuifanya mradi huu kusimama na kutotoa huduma tena kwa wananchi.
Aidha ilipofika mwaka 2019 mkandarasi alieharibu miundo mbinu hiyo ya maji aliweza kulipa fidia na ukarabati wa miundombinu hiyo kurejeshwa kama ilivyokuwa awali na huduma ya maji kuendelea kutolewa kwa wananchi tena.
Hivyo Wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) kwa kupitia mratibu wake ndugu Atunosyege Adamson Mwakang'ata, amekabidhi cheti kwa jumuia ya watumia maji ya Kijiji cha Lubaga ili kuifanya jumuia hiyo kuwa na nguvu ya kutumia sheria na miongozo ya uundaji wa jumuia za watumia maji vijijini sheria mpya iliyoundwa mwaka 2019.
Sheria hii imeundwa mahususi kwa lengo la kuwataka wananchi kumiliki miradi yao ya maji, hivyo wananchi hao walitunga katiba na kanuni zao zitakazowasaidia kutunza miradi yao ya maji isiweze kuharibiwa au kuhujumiwa na baadhi ya watu wasiopenda maendeleo.
Aidha akiongea kwa niaba ya wananchi mwenyekiti mpya wa jumuia ya watumia maji ya Kijiji cha Lubaga ndugu Deusi wiliamson Mwakabonga amesema, kwa upande wake yeye na jumuia yake wamejipanga katika kuhakikisha wanasimamia katiba na kanuni walizozitunga wenyewe ili kuifanya miradi ya maji kuwa endelevu na yenye tija kwa maendeleo ya wananchi wa kijijini hapo.
Mwisho mwenyekiti wa kijiji cha Lubaga ndugu Kumbuka Mwalubanga, alitoa shukrani zake za dhati kwa serikali ya awamu ya tano kwa kuwasimamia wananchi wa kijiji cha Lubaga na hatimae kuweza kurudishiwa huduma yao ya maji tena, hata hiyo mwenyekiti huyo hakusita kuiomba serikali kuwafikishia umeme katika chanzo chao cha maji, ili kuwapunguzia gharama za mafuta kwani kwa sasa wanatumia kangakevu katika chanzo chao cha maji.
Habari na Mawasiliano
Kyela.
Bomani Street
Sanduku la Posta: P. O box 320 Kyela
Simu ya Mezani: 025-2540035/7
Simu ya Mkononi: 0713655466
Barua pepe: ded@kyeladc.go.tz
Haki miliki @2017 Halmashauri ya wilaya ya Kyela. Haki zote zimehifadhiwa