Wataalamu wa Idara ya Afya kutoka Malawi na Wataalam wa Afya kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kyela kwa kushirikiana na taasisi ya Amref Health Africa nchini Malawi, wamefanya mkutano wa pamoja(cross border meeting) uliofanyika tarehe 02.07.2025 katika ukumbi wa Palazzo, kata ya Matema, wilayani Kyela.
Lengo kuu la mkutano huo ni kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Malawi katika mapambano dhidi ya magonjwa hatari ya mlipuko yanayoathiri nchi zote mbili, hasa maeneo ya mipakani. Washiriki waliangazia umuhimu wa kuwa na mifumo imara ya ufuatiliaji na udhibiti wa milipuko kabla haijasambaa kwa kasi.
Mkuu wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Wilaya ya Kyela, Dkt. Saumu Kumbisaga, alitoa shukrani kwa Amref Health Africa kwa kushiriki na kuchangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha mkutano huo muhimu.
Dkt. Kumbisaga pia aliwapongeza washiriki wa mkutano kwa kutoa maoni yenye tija ambayo, kwa pamoja, yatawezesha upatikanaji wa suluhu za kujikinga na kudhibiti magonjwa ya mlipuko, hasa kwa jamii zinazokaa maeneo ya mipakani.
Kwa upande mwingine, Afisa Afya Mazingira wa Wilaya ya Karonga nchini Malawi, Ndg. Owner Nguhube, alitoa shukrani kwa niaba ya wataalamu kutoka Malawi. Alisifu ukarimu wa uongozi wa Tanzania, hasa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, kwa mapokezi mazuri na ushirikiano waliouonyesha.
Ndg. Nguhube alieleza kuwa mkutano huo ni jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu mbalimbali za kisayansi na kijamii zitakazosaidia kuzuia magonjwa ya mlipuko pande zote mbili za mpaka wa Malawi na Tanzania.
Bomani Street
Sanduku la Posta: P. O box 320 Kyela
Simu ya Mezani: 025-2540035/7
Simu ya Mkononi: 0713655466
Barua pepe: ded@kyeladc.go.tz
Haki miliki @2017 Halmashauri ya wilaya ya Kyela. Haki zote zimehifadhiwa