Katibu Tawala wa Halmashauri ya wilaya ya Kyela Bi. Sabrina Humoud Ruhwey amezindua zoezi la Ugawaji wa Vyandarua katika shule za msingi wilayani Kyela, Zoezi hilo limefanyika leo tarehe 20/11/2023 katika shule ya msingi Kyela.
Akizindua zoezi hilo, Bi. Sabrina Humoud Ruhwey amewataka walimu wa shule ya Msingi Kyela kuhakikisha Watoto wote wa shule hiyo wanapata vyandarua, kama itakavyofanyika kwa watoto wa shule za msingi kuanzia darasa la kwanza mpaka darasa la 6.
Pamoja na hayo, Bi. Sabrina Ruhwey amesema wanagawa vyandarua kwa lengo la kupambana na Malaria wilayani Kyela, pia amewataka wazazi wa kuhakikisha wanatumia vyandarua hivyo kwa matumizi sahihi. Na si kwa shughuli nyingine za kijamii kama vile uvuvi wa samaki, kuweka uzio wa Bustani au kwa ufugaji wa kuku kwani kwa kufanya hivyo, kutadhoofisha vita dhidi ya Malaria.
Hata hivyo Bi. Sabrina Humoud amewatoa hofu wazazi kuwa vyandarua hivyo ni salama kabisa kwa binadamu, na havina madhara yeyote ya Kiafya kwa binadamu.
"kama watu wengine wenye dhana potofu wasemavyo kuhusu vyandarua hivyo kuwa vinapunguza nguvu za uzazi kitu ambacho hakina ukweli wowote kwani vyandarua hivyo vimepimwa na wataalamu wa afya kabla havijaruhusiwa kuingia nchini na kuanza kugawiwa" amesema Bi. Sabrina
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kyela ndg. Florah A. Luhala amewakumbusha wazazi kuchangia pesa ya chakula ili watoto waweze kupata chakula shuleni.
Bi. Florah Luhala ameongeza kuwa Siyo jambo zuri kwa watoto wachache kupata chakula na wengine kukosa chakula, kwa kuwa hawajachangia pesa ya chakula, kwani kufanya hivyo ni kunatengeneza chuki na utengano baina ya watoto.
Vilevile Bi. Florah Luhala amesema watoto wakipata chakula wote kwa pamoja shuleni kuna tengeneza Upendo na Mshikamano, jambo ambalo hupelekea watoto Kusaidiana katika masomo na kurahisisha ufaulu mashuleni.
"Haileti picha nzuri watoto wengine wanakula wakati watoto wengine wamekaa pembeni wakiangalia wenzao wakila eti kwasababu hawajachangia, unaweza ukaona ni jambo la kawaida lakini siyo la kawaida kwa watoto, tunawaharibu ufahamu wao" Amesema Bi. Florah
Aidha Bi. Florah Luhala amehitimisha kwa kuwataka wazazi kuzingatia malengo ya vyandarua vilivyogawiwa na amewaomba wazazi wakavitumie kama ilivyopangwa.
Bomani Street
Sanduku la Posta: P. O box 320 Kyela
Simu ya Mezani: 025-2540035/7
Simu ya Mkononi: 0713655466
Barua pepe: ded@kyeladc.go.tz
Haki miliki @2017 Halmashauri ya wilaya ya Kyela. Haki zote zimehifadhiwa